96% DARASA LA SABA KUJIUNGA SEKONDARI


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini akitangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2014 ofisini kwake Dar es Salaam jana. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia Elimu.
ASILIMIA 96.15 ya wanafunzi wa darasa la saba waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu na kufaulu, ndio waliochaguliwa kujiunga na sekondari za serikali.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI, Jumanne Sagini aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kwamba jumla ya wanafunzi 411,127 kati ya 427,609 waliofaulu mtihani huo ndio watakaoanza kidato cha kwanza mwakani.
Alisema wasichana ni 201,021 na wavulana 210,106 na kwamba waliochaguliwa wameongezeka kwa asilimia 31.37 ikilinganishwa na asilimia 64.78 waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka huu.
Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani mwaka huu, alama ya juu kabisa kwa wavulana ilikuwa 244 huku ya wasichana ikiwa ni 241 kati ya alama 250 ambapo mwaka jana alama ya juu ilikuwa 237.
“Matokeo yanaonesha kuwa jumla ya wanafunzi 427,609 (wavulana 218,093 na wasichana 209.516) walifaulu kwa kupata alama A-C kati ya 844,938 waliofanya mtihani ikiwa ni sawa na asilimia 50.61 … takwimu zinaonesha ongezeko la asilimia 19 la ufaulu ikilinganishwa na asilimia 30.6 mwaka jana,” alisema Sagini.
Kuhusu udanganyifu katika mtihani, Katibu Mkuu alisema takwimu zinaonesha waliofutiwa matokeo kutokana na udanganyifu imepungua mwaka huu kwa kuwa na wadanganyifu 13 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo waliofutiwa walikuwa 219.
Alisisitiza msimamo wa Serikali kuwachukulia hatua stahiki watendaji watakaobainika kujihusisha na udanganyifu katika mitihani.
“Vitendo hivyo vinatoa taswira mbaya kwa Taifa na kufanya watoto wetu wawe tegemezi zaidi kuliko kujituma na kujibidiisha katika masomo yao,” alisema na kuwataka walimu, wazazi na jamii kwa jumla kujiepusha na vitendo hivyo.
Pamoja na kushukuru walimu, walimu wakuu, kamati za shule, waratibu wa elimu kata, viongozi wa halmashauri, sekretarieti za mikoa na wadau wa elimu nchini kwa ushirikiano wao wa kusimamia elimu, aliasa waliochaguliwa kutumia fursa hiyo vizuri.
Aliagiza walimu na watendaji wa elimu katika ngazi zote kuongeza bidii katika ufundishaji, usimamizi na ufuatiliaji wa kutoa elimu ili kuinua ubora wa elimu nchini.
Alitaka pia ukamilishaji majengo na mazingira ya kupokea wanafunzi wote waliochaguliwa na kuhakikisha wanaandikishwa, wanahudhuria na kubaki shuleni hadi watakapohitimu masomo yao ya sekondari.
“Naziagiza halmashauri zilizobakiza wanafunzi 16,482 katika awamu ya kwanza ya uchaguzi kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 412 ili kuwezesha wanafunzi hao kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Machi.
Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifanyika Septemba 11 na 12 kwa kutumia teknolojia mpya ya OMR ambapo mitihani ilisahihishwa kwa kompyuta.
Jumla ya wanafunzi 867,983 walisajiliwa kufanya mtihani, wasichana wakiwa 455,896 ambapo 844,938 ndio waliofanya mitihani hiyo huku 23,045 wakikosa kuifanya kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za utoro, vifo na ugonjwa.
CHANZO CHA HABARI NI HABARI LEO


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...