Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Fraisser Kashai |
MTU mmoja mkulima na mkazi wa eneo la
Kumsenga wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, aliyefahamika kwa jina la Yusuph
Pascal, ameuawa kwa kupigwa na vitu mbalimbali katika tukio linalodaiwa kuwa ni
fumanizi la mapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Fraisser
Kashai alisema kwamba mtuhumiwa huyo wa fumanizi, aliuawa mwanzoni mwa wiki
hii.
Alisema baada ya kifo chake, mume wa mwanamke
aliyefumaniwa kwa kushirikiana na watu wengine, waliuchukua mwili wa marehemu
na kuutupa eneo la Mnarani mjini Kasulu.
Kufuatia tukio hilo, kamanda huyo alisema
watu watano wanashikiliwa na jeshi hilo, wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo la
mauaji ya mkulima huyo.
Kashai aliwataja watu waliokamatwa kwenye
tukio hilo kuwa ni watu watatu wa familia moja, ambao ni Augustino Adrian,
Laurent Adrian na Peter Adrian, ambao ni wamiliki wa nyumba yalipotokea mauaji.
Aliwataja wengine waliokamatwa kuhusiana na
tukio hilo kuwa Mihosho Hamza, ambaye ni mume wa mwanamke aliyefumaniwa akiwa
ni mpangaji katika nyumba yalikotokea mauaji na Raymond Shirima.
Akisimulia kuhusu tukio, Mkuu wa upelelezi na
makosa ya jinai mkoa Kigoma, David Kisusi alisema awali marehemu akiwa katika
nyumba ambayo mwanamke aliyefumaniwa naye alikuwa akiishi, alivamiwa na
watuhumiwa, ambao walimpiga na vitu vizito na kufariki.
Alisema baada ya kuona kuwa mtuhumiwa huyo wa
fumanizi ameuawa, mume wa mwanamke huyo na watuhumiwa wengine wanne,
waliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuutupa eneo la Mnarani ili kupoteza
ushahidi.
Alisema polisi walipofika eneo ambalo mwili
huo wa marehemu ulikuwa umetupwa, walianza uchunguzi wao na kubaini kuwa
ulitupwa hapo baada ya kuuawa eneo lingine.
Ndipo walipofuatilia michirizi ya damu hadi
katika nyumba hiyo na kukuta katika moja ya vyumba hivyo, kuna eneo limemwagiwa
mchanga mwingi ili kuficha damu hiyo ya marehemu.
Habari Leo