Kutoka Kushoto mawaziri, Kawambwa, Kombani, Chiza, Matayo na Ghasia
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) imekutana jana mjini hapa chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, na kuanza kuwahoji mawaziri wanaodaiwa kuwa mzigo kwenye Baraza la Mawaziri.
Kamati hiyo iliyoanza kikao chake majira ya saa 5 asubuhi katika jengo la White House, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ilikuwa na agenda kadhaa, ikiwamo kuu ya kuwajadili mawaziri hao.
Suala la mawaziri hao kuwa mzigo, limekuwa gumzo hasa katika vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini hapa na kusababisha baadhi ya wabunge kutaka mawaziri hao wachukuliwe hatua.
NIPASHE Jumamosi ilishuhudia baadhi ya mawaziri waliotajwa kuwa mzigo wakiwa katika viwanja vya White House, wakisubiri kuitwa kwa mahojiano.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Celina Kombani, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. Mathayo David.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Mawaziri hao waliitwa na Kamati kuu kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na kulalamikiwa kuwa utendaji wao ni mbaya.
Mpaka gazeti hili linaenda mitamboni, mawaziri wawili akiwamo Kombani na Kawambwa, walikuwa wameshaitwa na kuhojiwa.
Mapema kabla ya kikao hicho kuanza, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipohojiwa na waandishi kuhusu agenda zitakazojadiliwa kwenye kikao hicho, alisema taarifa kamili zitatolewa leo.
Hata hivyo, NIPASHE Jumamosi ilishuhudia mawaziri hao wawili wakiwa tayari wameshahojiwa wakiwa nje ya ukumbi.
Hivi karibuni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nnauye, mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa mawaziri hao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Kauli hiyo aliitoa wakati viongozi hao wa chama walipofanya ziara katika mikoa mbalimbali ya kusikiliza kero za wananchi kwa nia ya kukiimarisha chama.
Alionyesha kusikitishwa kwake na kitendo cha mawaziri hao waliopewa dhamana kushindwa kutambua wajibu wao na kueleza kuwa umefika wakati wa wao kuhojiwa na Kamati Kuu ya chama ili wachukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo aibu itarudi kwa chama chake.
Nape alitoa kauli hiyo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati akielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Hisani ya Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)