Maaskofu wa Makanisa mbalimbali mchini, wamezungumzia kwa nyakati
tofauti mustakabali wa Taifa huku wakitaka watawala kuheshimu maoni
yaliyotolewa na wananchi kuhusu Katiba mpya pamoja kuchukua hatua mapema
kwa viongozi waliopewa dhamana za kuongoza na kushindwa kuwajibika.
Katika mahubiri yake kwenye Kanisa Kuu la Utatu Mtakatifu, Askofu
Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Seheba,
alitaka watawala kuheshimu mapendekezo yote yalitolewa katika rasimu ya
pili ya Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Askofu Seheba alisema kuwa mapendekezo hayo yaliyotolewa na wananchi
iwapo yataheshimiwa na kupitishwa katika Bunge la Katiba, yatasaidia
kuleta umoja na mshikamano ili kuifanya nchi kuwa na amani na utulivu
kama ilivyokuwa na sifa yake.
Hata hivyo, Askofu Seheba alisisitizia umuhimu wa Watanzania
kuendelea kuombea rasimu hiyo ili ipatikane kwa Katiba mpya itakayokidhi
mahitaji ya Watanzania kwa maslahi ya nchi na ustawi wa jamii.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Jimbo la
Morogoro, Jacob Mameo, akizungumza katika mahubiri yake katika Kanisa la
Mji mpya, alisema mwaka 2014, uwe ni mwaka wa serikali kuchukua hatua
za haraka kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza na kushindwa
kuwajibika badala ya kusubiri madhara kujitokeza kwa wananchi.
Askofu Mameo alisema mwishoni mwa mwaka jana, Taifa lilishuhudia
madhara makubwa waliyopata wananchi wakati wa Operesheni Tokemeza
kutokana na viongozi hao waliopewa mamlaka kushindwa kusimamia ipasavyo.
Alisema hali hiyo isipodhibitiwa mapema itazidi kuleta athari kwa
wananchi. Askofu Mameo aliwataka viongozi wanaopewa dhamana kuwa na hofu
ya Mungu katika utendaji wao wa kazi na kuweka maslahi ya taifa mbele
ili kuleta maendeleo na kudumisha amani iliyopo.
Kwa upande wake, Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la
Morogoro, Telesphori Mkude, alisisitiza umuhimu wa waumini wa dini zote
kuendelea kuliombea Taifa ili kuwa na amani hasa katika kipindi hiki cha
mchakato wa kupata Katiba mpya.
Askofu Mkude aliwataka Watanzania kuepuka mifarakano na uvunjifu wa
amani na badala yake wawe kitu kimoja hasa katika kipindi hiki cha
kuibuka kwa rasilimali mbalimbali za taifa ikiwamo gesi na mafuta.
–NIPASHE–