Naibu
Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia nishati, Mhe. Charles
Kitwanga katikati akisisitiza jambo wakati wa kikao na Mameneja wa
Tanesco wa wilaya katika Mikoa ya Mtwara na Lindi (hawapo pichani).
Pamoja nae ni watendaji wakuu wa Tanesco Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kikao hicho kilijadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha
umeme vijijini kupitia REA na namna ya kuvifikia vijiji ambavyo
havijafikiwa katika utekelezaji wa mradi huo awamu ya pili.
Baadhi
ya Mameneja wa Tanesco wa Wilaya katika Mikoa ya Lindi na Mtwara
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati nayeshughulikia Nishati Mhe.
Charles Kitwanga (hayupo pichani) wakati wa kikao. Mhe. Kitwanga
alisisitiza ubunifu na kuhakikisha mameneja hao wanapunguza tatizo la
kukatikakatika kwa umeme katika Mikoa hiyo.
Kaimu
Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme cha Tanesco- Mtwara Mhandisi Didas
Maleko ( wa pili kulia) akimwongoza Naibu Waziri wa Nishati na Madini
(Nishati) Mhe. Charles Kitwanga kuangalia mitambo inayozalisha umeme
katika kituo hicho. Kwa mujibu wa maelezo ya Maleko, kituo hicho kina
uwezo wa kuzalisha kiasi cha megawati 18.
Mhe.
Naibu Waziri akitoka kuangalia maendeleo ya ujenzi wa bomba katika eneo
la Somanga. Nyuma linaloonekana ni sehemu ya bomba la gesi la nchi 36
ambalo linaelekea Dar es Salaam katika eneo la Kinyerezi likitokea
Mtwara.
Msimamizi wa Kituo cha kuzalisha umeme wa gesi asilia cha Somanga Mhandisi.
======== ======= ======
Na Asteria Muhozya, Mtwara
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Mhe. Charles
Kitwanga, amewataka wananchi waliopo katika vijiji vinavyopitiwa na
Mradi wa kuunganisha Umeme Vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Umeme
vijijini (REA) kuchangamkia fursa hiyo wakati ambao mradi huo
unatekelezwa kwa kuwa gharama zake ni nafuu.
Mhe.
Kitwanga aliyasema hayo jana wakati wa kikao chake na Mameneja wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Wilaya za Lindi na Mtwara
waliokutana kwa lengo la kujadili maendeleo ya mradi wa kuunganisha
umeme Vijijini katika Wilaya za mikoa hiyo unaosimamiwa na REA, ikiwa
ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kuvifikia vijijii
ambavyo bado havijafikiwa na mradi huo awamu ya pili.
Aliongeza
kuwa, wananchi walioko katika maeneo ya vijiji ambapo mradi wa REA
awamu ya pili unatekelezwa, wanapaswa kuitumia fursa hiyo vizuri kwa
kuwa gharama kubwa za kuunganisha umeme zimebebwa na serikali kwa
kipindi hicho na endapo mradi huo utakapokamilika watatakiwa kulipa
gaharama zote kama kawaida.
Aidha,
alizitaja gharama hizo kwa kipindi cha utekelezaji wa mradi wa REA
awamu ya pili kuwa ni kiasi cha shilingi 27,000/- ikiwa ni gharama ya
kuunganishwa ambayo ni VAT na gharama za fomu kiasi cha shilingi
5000/-
Katika
hatua nyingine Mhe. Kitwanga aliwataka Mameneja wa Tanesco kuhakikisha
wanapunguza tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika Mikoa ya Lindi na
Mtwara na kuhakikisha wanaweka mipango endelevu ya upatikanaji wa
nishati hiyo kutokana na kwamba mikoa hiyo inatarajia kuwa na uwekezaji
mkubwa vikiwemo viwanda vya sementi.
Aidha,
aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu na kuongeza kasi ya utendaji
katika shughuli zao ili kurejesha imani ya wananchi kuhusu shirika hilo
kwa kuzingatia kwamba, nishati hasa umeme ina mchango mkubwa katika
shughuli zote za kiuchumi na maendeleo ya taifa.
“Lazima
tuibadilishe Tanesco. Wananchi wanatakiwa waishangae tanesco kwa huduma
nzuri na si vinginevyo. Sitaki umeme ukatike hovyo hovyo. Vaeni viatu
mlivyopewa.Taswira ya tanesco lazima ibadilike”. Aliongeza Kitwanga.
Halikadhalika,
aliwataka mameneja hao kuhakikisha wanakusanya madeni kutoka kwa
wadaiwa wote zikiwemo taasisi za serikali na watu binafsi ili kuwezesha
shirika hilo kujiendesha na kuendelea kutoa huduma kwa wananachi. Hivyo,
amewataka wateja wote wanaodaiwa na shirika hilo kuhakikisha wanalipa
madeni yao ili shirika hilo liendee kutoa huduma stahiki.
Wakati
huo huo, Meneja Mwandamizi wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani,
Mhandisi Mahenge Mugaya alieleza kuwa, tatizo la kukatikakatika kwa
umeme katika mikoa hiyo linaweza kuzuilika na kuongeza kuwa, tayari
zoezi la kubadilisha nguzo mbovu limeanza na kuwekwa mpya. Vilevile,
aliongeza kuwa, katika kukamilisha zoezi hilo, tayari watumishi zaidi
wameongezwa kutoka Dar es Salaam kwa ajili ya shughulli ya kubadilisha
nguzo hizo.
Kwa
upande wake Kaimu Meneja wa Kituo cha Tanesco- Mtwara cha kuzalisha
umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara , Mhandisi Didas Maleko, wakati
akitoa taarifa ya uzalishaji umeme katika kituo hicho alieleza kuwa,
kituo hicho kinazalisha kiasi cha megawati 18 kutoka katika mashine
tisa ambapo kila machine inazalisha kiasi cha megawati 2.
Katika
hatua nyignine Mhe. Kitwanga alitembelea eneo la wazi la makutano ya
bomba la gesi la inchi 16 kutoka Songosongo na lile la inchi 36
linalotoka Mtwara kwenda Kinyerezi Dar es Salaam katika eneo la
Somangafungu ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo. Aidha,
alitembelea kituo cha kuzalisha umeme unaotokana na gesi asilia kilichopo Somangafungu ,kituo ambacho kina uwezo wa kuzalisha megawati 7.5.