Uongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), umetangaza kurejea kwa Gazeti la Mwananchi mitaani na kuushukuru umma kwa kuwa nao bega kwa bega katika kipindi lilipofungiwa na Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Tido Mhando alisema kwa mujibu wa agizo la
Serikali la kutochapishwa kwa Gazeti la Mwananchi, adhabu ilimalizika
jana.
Mhando alisema kuanzia leo gazeti litakuwa mitaani
kama kawaida na kuwaahidi wasomaji kuwa wataendelea kupata gazeti lenye
habari za uhakika zinazojikita kwenye umahiri, uhuru, weledi wa
uandishi na uhariri.
“Ni dhamira yetu siku zote kuwapatia wasomaji wetu kile wanachostahili, kwa namna wanayostahili kukipata,” alisema Mhando.
Alisema gazeti hili litaendelea kusambazwa nchi
nzima na kufika mapema kabisa kupitia kwa mawakala na wauzaji walioenea
kote nchini.
Pia alisema katika wiki mbili za kufungiwa kwa
Gazeti la Mwananchi, jumuiya ya wafanyabiashara, taasisi na watu
mbalimbali waliathirika kwa kukosa fursa ya kutangaza.
“Wateja wetu walizoea kutangaza na wanaridhishwa
na huduma zetu. Huku tukiwapa pole, tunawakumbusha kwamba sasa tunarejea
kwa ajili ya kuwahudumia na tumejipanga,” aliongeza Mhando.
Gari la mshindi wa Chomoka
Mshindi wa gari la kwanza la Mwananchi katika droo
ya Promosheni ya ‘Chomoka na Mwananchi’ ambaye alikuwa ni Benedict Ngoo
mkazi wa Dodoma, atakabidhiwa gari lake Jumatano ijayo.
Ngoo atakabidhiwa zawadi yake wakati gazeti hili likiwa limerejea mitaani baada ya kufungiwa kwa siku 14 na Serikali.
Meneja Masoko wa MCL, Bernard Mukasa alisema jana
kuwa gari hilo litakabidhiwa kwa mshindi huyo ambaye ni mfanyakazi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Dodoma, katika hafla
itakayofanyika jijini Dar es Salaam.
“Ngoo atakabidhiwa gari lake wiki ijayo lakini
napenda kuwakumbusha wasomaji wetu kuwa magari mawili yamebaki kwa ajili
ya kushindaniwa,” aliongeza Mukasa.
Siku hiyo pia washindi wa kila siku wa Sh1 milioni, waliopatikana kabla ya gazeti halijafungiwa, watakabidhiwa zawadi zao.
Mshindi huyo wa gari alipatikana Septemba 23 mwaka
huu katika droo ya kwanza ya gari iliyofanyika baada ya siku 30 za
promosheni hiyo ya siku 100.
“Ngoo alikuwa miongoni mwa watu 465,000
walioshiriki katika droo hiyo kwa ajili ya kushindania zawadi
mbalimbali,” alisema Mukasa.
Washiriki katika droo hiyo wanatakiwa kutuma namba
zilizopo katika jarida la ndani la Gazeti la Mwananchi kwenda katika
namba 15584.
Mukasa alisema droo za kila siku zinaendelea na
kesho mshindi wa 38 wa Sh1Milioni wa Chomoka na Mwananchi, atapatikana
baada ya kuchezeshwa kwa droo katika ofisi za gazeti hili zilizopo jengo
la JMall jijini Dar es Salaam.
MWANANCHI
MWANANCHI