MANDELA; HAITATOKEA TENA!

Jeneza lenye mwili wa Mandela likiwa eneo la makabauri tayari kwa mazishi.
Stori: Mwandishi wetu
RAIS wa kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini huru, Nelson Mandela alizikwa juzi katika kijiji alichokulia cha Qunu, Mthatha katika jimbo la Eastern Cape na kutoa picha kwamba haitatokea tena kwa rais mwingine yeyote wa Afrika.

 
Nelson Mandela enzi za uhai wake.
Mandela alizikwa siku kumi baada ya kufariki akiwa nyumbani kwake jijini Johannesburg, akihitimisha tukio kubwa kabisa la kihistoria kuwahi kutokea barani Afrika, kwa viongozi wote wa mataifa makubwa kuhudhuria siku maalum ya maombolezo iliyofanyika katika Uwanja wa FNB huko Soweto.
Mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela, akiangalia jeneza la babu yake wakati wa shughuli za mazishi kijijini Qunu.
Pia viongozi hao, wakiongozwa na Rais Barack Obama wa Marekani, walishiriki katika kuuaga mwili wa mpiganaji huyo katika Majengo ya Umoja jijini Pretoria, ambako pia zaidi ya waombolezaji laki moja walipita na kutoa heshima zao za mwisho kwa Mandela.
Serikali ilitoa amri ya kusitishwa kwa shughuli ya kuaga mwili huo wakati idadi ya wananchi wapatao 50,000 wakiwa bado katika foleni.
Wakati wa ibada za mazishi yake zilizofanyika kidini, kiserikali na kimila, wageni waalikwa 4500 tu waliruhusiwa kushiriki tukio hilo, wakiwa wamekusanyika katika hema kubwa lililojengwa katika eneo la familia yake huko Qunu.
Katika historia ya Afrika ni kiongozi pekee aliyeweka rekodi ya kuwakutanisha viongozi wa mataifa makubwa, maadui na marafiki katika tukio moja kama ilivyokuwa Afrika Kusini.
Kwa jinsi viongozi wa bara hili wanavyoishi na kufanya kazi, ni jambo lisilofikirika kuifikia rekodi hiyo.

Katika hafla ya mazishi hayo yaliyohudhuriwa na marais wawili tu ambao wote walihutubia, Jakaya Kikwete wa Tanzania alikuwa kivutio, baada ya hotuba yake kuwasisimua mamia ya waombolezaji, ambao pia walilazimika kumshangilia mara kwa mara alipokuwa akielezea historia ya marehemu na jinsi alivyojenga uhusiano wa kindugu na Tanzania.
Licha ya marais hao, pia rafiki wa karibu wa Mandela, rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton na Prince Charles wa Uingereza pia walihudhuria, sambamba na mwendeshaji wa kipindi cha televisheni maarufu wa Marekani, Ophrah Winfrey aliyekuwa na mumewe.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...