TUME YA KATIBA KUKABIDHI RASIMU YA PILI DESEMBA 30

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakabidhi rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka huu.
Makabidhiano hayo yatafanyika katika hafla itakayofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam baada ya Tume kumaliza kazi yake ya kuiandaa.
Rasimu hiyo ya pili inatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa rasimu ya kwanza ya ambayo ilijadiliwa katika Mabaraza ya Katiba yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ibara ya 20 (2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mara baada ya Rais kukabidhiwa rasimu hiyo, itachapishwa katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine ndani ya siku 31.

Pia katika kipindi hicho, Rais anatakiwa kuitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu iliyopendekezwa. Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa Bunge la Katiba litaanza vikao vyake Februari, 2013.

Taarifa ya Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid iliyotolewa jana ilieleza kuwa Tume hiyo itakabidhi rasimu hiyo kwa Marais Kikwete na Dk Shein katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na wananchi wa kawaida.

Tume hiyo ilitakiwa kumaliza kazi ya kuandaa rasimu ya pili Desemba 15 mwaka huu lakini Rais Kikwete aliiongezea siku 14 zaidi hadi Desemba 30, mwaka huu.

Hatua hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume hiyo ilikuwa ya pili. Mara ya kwanza iliomba kuongezewa muda wa siku 45, kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu. Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 30.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza Tume hiyo kufanya kazi kwa miezi 18 licha ya kuwa inampa Rais mamlaka ya kuiongezea muda usiozidi siku 60.

Hatua ya Rais kuiongezea muda kwa mara ya pili, ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa wajumbe wake kujipanga upya baada ya kifo cha mwenzao, Dk Sengondo Mvungi kilichotokea Novemba 12, mwaka huu huko Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga.

Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotolewa Juni 4, mwaka huu.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...