BUNGE LA BAJETI: BALOZI ZIAJIRI MAOFISA UTALII, SARAKIKYA KIKAANGONI


Anne Makinda akiongoza bunge.
MBUNGE wa Bariadi Mashariki kupitia chama cha DP, John Cheyo, amezitaka balozi za Tanzania nje ya nchi, kuajiri maofisa wa utalii ambao kazi yao kubwa itakuwa ni kuwashawishi wageni mbalimbali kutembelea nchini na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo.
Alitoa ushauri huo wakati akitoa mchango wake katika mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma.
Paul Sarakikya kikaangoni
Mkurugenzi wa Idara za Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii Paul Sarakikaya amejikuta katika kikaango kikali bungeni, baada ya mbunge mmoja kumtaka Waziri Lazaro Nyalandu kueleza sababu za kumrejesha katika nafasi yake, licha ya jina lake kuwa miongoni mwa maofisa ambao walipendekezwa na Kamati ya Bunge kutimuliwa kazi kwa vile utendaji wao ni wa kutiliwa shaka.

Hifadhi zinawaua watu wa Karatu
Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse amemlalamikia Waziri wa Maliasili na Utalii kuwa licha ya neema ya wananchi wao ya kupakana na hifadhi za wanyama za Ngorongoro, lakini maisha yao yapo hatarini, kwani licha ya kuharibiwa kwa mashamba yao mara kwa mara kunakofanywa na wanyama hatari, pia baadhi ya watu huuawa na wanyama hao, hasa Tembo na Nyati.

Alisema kilio cha wananchi hao ni cha kila mwaka, lakini Wizara imekuwa kimya bila kujua kuwa endapo wananchi hao wataamua kujilinda wao na mazao yao, kunaweza kutokea jambo baya ambalo asingependa litokee.
Pembe za Tembo wizarani zichomwe
Mbunge wa viti maalum wa Chama Cha Mapinduzi Betty Machangu ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuzichoma moto shehena ya meno ya Tembo yaliyohifadhiwa wizarani hapo ili kuionyesha dunia kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kutokomeza biashara haramu ya bidhaa hiyo.

“Ili dunia ijue kuwa sisi hatutaki biashara hii, basi nashauri zile pembe zilizopo pale Ivory room zichomwe moto, tena ifanyike sherehe kabisa na kila kitu kiwe wazi,” alisema mbunge huyo.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...