Marehemu Dunia Mzobora enzi za uhai wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari,
Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia kifo
cha Mwandishi wa Habari na Msanifu wa Habari Msaidizi Mkuu wa Gazeti la
Uhuru, Bwana Dunia Mzobora, kilichotokea tarehe 27 Novemba, 2013 katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu
ya shinikizo la damu.
Marehemu aliajiriwa katika Magazeti ya Uhuru na Mzalendo mwaka 1989
kama Mwandishi wa Habari Mwanafunzi, kisha akaendelea kupanda ngazi
hadi kufikia cheo cha Msanifu wa Habari na hatimaye kuwa Msanifu Mkuu
Msaidizi, cheo alichokuwa akikishikilia hadi mauti yalipomkuta.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa
Waandishi wa Habari Shupavu na Mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa
akilitumikia Gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU,
kilichosababishwa na ugonjwa wa shinikizo la damu baada ya kuwa
amepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu”,
amesema kwa masikitiko Rais Kikwete.
Rais Kikwete amesema binafsi alimfahamu vyema Marehemu Dunia
Mzobora, enzi za uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma vilivyo
katika kazi zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha Umma kwa
kutumia vyema kalamu yake, na kwa kuzingatia kikamilifu Maadili ya
Taaluma yake ya Uandishi wa Habari.
“Kufuatia taarifa za kifo cha Dunia Mzobora, ninakutumia wewe
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella
Mukangara na Wafanyakazi wote wa Kampuni ya Magazeti ya Chama ya Uhuru
na Mzalendo na kwa kweli Waandishi wote wa Habari nchini, Salamu zangu
za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Waandishi wa Habari Mahiri ambaye
amelitumikia vyema Taifa lake kupitia Tasnia ya Habari”.
“Aidha kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi
na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza
Baba, Kiongozi na Mhimili wa Familia”.
Rais Kikwete amewahakikishia Wanafamilia kuwa yeye binafsi yuko
pamoja nao katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, na anamuomba Mwenyezi
Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya
Marehemu Dunia Mzobora, Amina.
Rais Kikwete amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira
katika kipindi hiki kigumu wanachopitia baada ya kumpoteza mtu muhimu
aliyekuwa kiungo cha Familia yao, kwani yote ni Mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.