Zimebaki
siku chache kabla ya kuuaga mwaka 2013, mwaka ambao umekuwa na matukio
mengi yaliyoitikisa nchi ya Tanzania, huku mengine yakiipa sifa kubwa.
Historia
ya Tanzania kuwa na Katiba Mpya itakayopatikana kutokana na maoni ya
wananchi ilianza Desemba 31, 2011 wakati Rais Jakaya Kikwete
akilihutubia taifa, alikiri wazi kuwa sasa inahitajika Katiba Mpya ili
kuendana na wakati wa sasa.
Baadaye
Rais Kikwete aliwateua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba na ilianza kazi yake ya miezi 18,
kuanzia Mei 3, mwaka 2012.
Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na kuandaa rasimu ya kwanza ya Katiba ambayo iliitoa Juni 4, mwaka huu.
Baada
ya kutolewa kwa rasimu hiyo wananchi walipewa muda wa kuipitia na
kuitolea maoni katika Mabaraza ya Katiba ya wilaya, yaliyokaa kuanzia
Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Maoni
hayo yalikusanywa na tume hiyo kwa ajili ya kuyachambua na kutoa rasimu
ya pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kutolewa Desemba 30, mwaka huu.
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilitakiwa kumaliza kazi ya kuandaa rasimu ya pili
Desemba 15, mwaka huu, lakini Rais Kikwete aliiongezea siku 14 zaidi na
hivyo kuifanya iweze kuendelea na kazi hadi Desemba 30.
Hatua
hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume hiyo ilikuwa ya pili, kwani
mara ya kwanza tume hiyo iliomba kuongezewa muda wa siku 45, kuanzia
Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu.
Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, tume ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 30.
Kwa
uamuzi wake, wa kuiongezea Tume hiyo siku nyingine 14, Rais Kikwete
ameiongezea tume hiyo jumla ya siku 59 kati ya 60 ambazo anaruhusiwa
kisheria.
Kifo cha Dk Sengondo Mvungi
Hatua
ya Rais kuiongezea muda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitafsiriwa kama
kutoa fursa kwa wajumbe wa tume hiyo kujipanga upya baada ya kifo cha
mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Dk Sengondo Mvungi aliyefariki dunia
Novemba 12, mwaka huu nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya
kujeruhiwa kwa mapanga na watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi, nyumbani
kwake mkoani Dar es Salaam.
Ujio wa Rais wa Marekani Barack Obama
Ni siku
mbili za kihistoria ambazo zimeweka rekodi ya aina yake katika historia
ya nchi hii, kuanzia maandalizi ya ujio wake mpaka alivyowasili nchini
Julai 1 na kuondoa Julai 3, mwaka huu.
Shughuli
nyingi na barabara kadhaa zilifungwa ili kutoa nafasi kwa ugeni huo
mkubwa uliojumuisha familia yake, wafanyakazi wa ikulu, walinzi na
makachero wa usalama kutoka nchini Marekani.
Katika
ziara yake hiyo, Rais aliwekea mkazo umuhimu ambao Marekani inauweka
katika ushirikiano wetu wa kina na unaoendelea kuimarika na nchi za
Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mipango mbalimbali ikiwemo ile ya
kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara, uimarishaji wa
taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika kizazi kipya cha viongozi wa
Kiafrika.
Ziara ya Rais wa China, Xi Jinping
Ziara
hii ilitokea ikiwa ni wiki mbili tangu achaguliwe Xi Jinping kuwa Rais
wa China, ambapo aliichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitembelea
barani Afrika.
Katika
ziara hiyo Rais Jinping alikutana na viongozi mbalimbali nchini,
kusaini mikataba ya kidiplomasia 19, ukiwemo wa ujenzi wa Bandari
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akiwa
nchini Rais Jinping alitoa hotuba yake ya kwanza tangu achaguliwe
kushika wadhifa huo, ambayo iligusia masuala ya kiuchumi, kisiasa
sambamba na kueleza msimamo wa nchi yake kwa Tanzania na Afrika.
Rais
huyo alikutana pia na jumuiya ya watu wa China na kutembelea makaburi ya
wataalamu wa Kichina ambayo yapo Majohe, Ukonga ambako alitoa heshima
zake kwa Wachina waliofariki dunia wakati wakijenga reli ya Tazara.
Bomu la Arusha
Mei 5,
mwaka 2013 ni siku ambayo haitafutika katika historia ya Tanzania
kutokana na tukio la kusikitisha la kutupwa kwa bomu kanisani, ambapo
watu watatu walifariki dunia na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Tukio
hilo lilitokea mbele ya Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini
Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo, Askofu Mkuu Josephat Lebulu
wa Jimbo Kuu la Arusha, walipokuwa wakizindua jengo la Kanisa Katoliki,
Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.
Mgogoro wa gesi Mtwara
Maelfu
ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali
kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, kutoka mkoani hapo kwenda Dar es
Salaam.
Maandamano
hayo yaliyoratibiwa na vyama vya Chadema,CUF, NCCR-Mageuzi, Sau,
Tanzania Labour Party (TLP), APPT- Maendeleo, ADC, UDP na DP
yakishirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo, zikiwamo Tandahimba na
Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia
barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.
Kufuatia
fujo na vurugu zilizotokea katika maandamano hayo risasi na mabomu
yalirindima, hali iliyozua hofu na tafrani mkoani hapo.
Sakata la Sheikh Ponda
Tukio
la kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya ya Kiislamu nchini, Shekhe Ponda
Issa Ponda ilikuwa miongoni mwa habari zilizoibua mjadala mzito huku
kukiwepo na hali ya sintofahamu kama kiongozi alijeruhiwa kwa risasi au
kitu chenye ncha kali.
Mkasa
huo wa aina yake ulitokea Agosti 10, mwaka huu majira ya saa 12: 15 za
jioni eneo la Barabara ya Tumbaku karibu na Fire, mkoani Morogoro mara
baada ya kumalizika kwa Kongamano la Kiislamu lililofanyika kwenye
Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege, Kata ya Saba Saba.
Baada
ya tukio hilo, uvumi ulisambaa maeneo mbalimbali nchini ukidai kuwa
Shekhe Ponda amepigwa risasi na polisi na kufariki dunia.
Kuporomoka kwa ghorofa
Ilikuwa
ni asubuhi ya Machi 29 ambapo jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa
katika Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam, liliporomoka na
kusababisha vifo vya watu 36 na wengine kadhaa kufunikwa na kifusi.
Kuporomoka
kwa ghorofa hilo kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa
waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea hali
iliyosababisha kusimama kwa shughuli mbalimbali katikati ya jiji.
Matukio ya tindikali Mwaka 2013 kumekuwa na matukio mengi wa watu kumwagiwa tindikali hususan upande wa Zanzibar, ambapo matukio kadhaa yaliripotiwa.
Julai
19 mwaka huu Said Mohamed Saad ambaye ni Mkurugenzi wa Home Shopping
Center alimwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika kisha kutokomea na
kumuacha bilionea huyo katika maumivu makali.
Saad
alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu lakini ilishindikana
kutokana na madhara makubwa aliyoyapata kutokana na tindikali hiyo hali
iliyosababishwa kupelekwa Ujerumani kwa matibabu zaidi.
Matukio
mengine yalitokea Zanzibar kuhusisha raia wawili wa Uingereza, Kate
Gee na Kirstie Trup waliomwagiwa tindikali, eneo la Mji Mkongwe na Padri
wa Parokia ya Machui, Anselmo Mwang’amba .
Siku
chache baada ya tukio hilo lilitia doa nchi ya Tanzania katika ramani ya
kimataifa, jeshi la Polisi upande wa Zanzibar lilitangaza kukamata lita
29 za tindikali.
Mauaji ya kutumia silaha
Mwaka
huu pia kulikithiri kwa mauaji ya kinyama kwa kutumia silaha ambapo
watu kadhaa walijikuta wakipoteza maisha na wengine kujeruhiwa, kutokana
na vitendo hivyo vilivyoonekana kushika kasi nchini.
Miongoni
mwa matukio hayo ni mauaji ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya
Minara Miwili, Evarist Mushi ambaye alipigwa risasi na watu
wasiofahamika asubuhi ya Februari 17 mwaka huu.
Mauaji
mengine yalitokea Agosti 7 kwa mfanyabiashara maarufu wa madini Erasto
Msuya kuuawa kwa kupigwa risasi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro. Msuya
alikuwa anamiliki vitegauchumi kadhaa na kuaminika kama mfanyabiashara
aliyekuwa akiongoza kwa utajiri Mirerani aliuawa kwa kupigwa risasi
zaidi ya 20.
Tukio
lingine la mauaji lillilotokea Oktoba 13 eneo la Kibamba ambalo kwa
kiasi kikubwa lilihusishwa na ugomvi wa kimapenzi ambapo Mtangazaji wa
Kituo cha ITV, Ufoo Saro alijeruhiwa kwa risasi huku mama yake mzazi
akipoteza maisha kutokana na shambulio lililofanywa na mzazi mwenzie
aliyejulikana kama Anthery Mushi.
Operesheni Tokomeza
Operesheni hii iliyolenga kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya wanyamapori ilianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na mbuga za wanyama huku ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Idara ya Wanyamapori. Mawaziri wanne waliopoteza nafasi zao kufuatia operesheni hiyo, nao ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT).