
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani ametawazwa
 kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar na kusema 
ameshangazwa na mashambulizi ya tindikali dhidi ya viongozi wa dini 
Visiwani humo.
Akizungumza
 na waaandishi wa habari mara baada ya kutawazwa ndani ya Kanisa la 
Anglikana la Minara Miwili Mjini Unguja, Jaji Ramadhan amesema vitendo 
vya hujuma vinavyofanywa dhidi ya viongozi wa dini na Serikali ni 
kinyume na utamaduni wa Zanzibar.
Alisema 
Wakristo na Waislamu Zanzibar kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kama 
ndugu bila ya kubaguana kwa sababu za itikadi ya dini licha ya Waislamu 
kuwa asilimia 95.
Hata 
hivyo, alikumbusha kuwa wakristo wana mchango katika harakati za 
ukombozi wa Zanzibar, ambapo idadi kubwa ya waumini wake walianzisha 
Chama cha African Association mwaka 1935, ambapo rais wake wa kwanza 
alikuwa hayati, Mzee Augustino Ramadhan na baadaye akafuata hayati Mzee 
Abeid Amani Karume.
"Vitendo 
vya watu kumwagiwa tindikali vinanishangaza, sababu halisi siifahamu, 
najiuliza haya yametokea wapi, siyo jambo jema wala siyo sifa ya 
Zanzibar tokea enzi na enzi," alisema.
Alisema 
wakati umefika na kuwataka viongozi kuwa mstari wa mbele kukemea matukio
 ya hujuma za tindikali na uhalifu mwingine ikiwemo mashambulizi ya 
kutumia silaha za moto na watu kupotezewa maisha.
Jaji 
Augustino amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na Tanzania, Brigedia 
Jenerali wa JWTZ pia amewahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na
 Mahakama ya Afrika Mashariki, ambapo amesema kazi ya sheria 
hazitofautiani na kazi za kiroho kwa vile zote zinahitaji utende haki na
 kutimiza wajibu upasavyo. Kwa upande wake Askofu Philip Baji wa Chuo 
Kikuu cha Mtakatifu John cha Dodoma, alisema huu ni wakati mwafaka kwa 
Serikali kuwalinda viongozi wa dini bila ya kujali tofauti ya madhehebu 
yao kutokana na kukithiri kwa vitendo vya hujuma.
Chanzo:Mwananchi
 

 
