Makahaba mjini Nairobi Kenya waliungana na wenzao duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga unyanyasaji dhidi yao.
Waliandamana Jumanne kulalamikia kile wanachosema ni unyanyasaji
wanaofanyiwa na polisi pamoja na askari wa baraza la jiji wakati
wakiendesha biashara zao.
Walikusanyika katikati ya mji na kuelekea katika ofisi za baraza la jiji
kuwasilisha malalamiko yao wakisema kuwa wamechoka kuhangaishwa na
polisi na wanataka ulinzi.
Mwanaharakati wa maswala ya biashara ya ngono, John Mathenge
aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji, alisema kuwa wengi wao wameuawa na
kunyanyaswa hata na wateja wao pamoja na maafisa wa usalama.
Siku hii ya kimataifa, huadhimishwa kila mwaka tarehe 17.
Biashara ya ngono imeharamishwa nchini Kenya lakini baadhi ya
watetezi wa makahaba wanasema kuwa katiba haijaeleza bayana ikiwa mtu
atakayekamatwa akijihusisha na biashara hiyo achukuliwe hatua gani za
kisheria.
Mathenge alielezea kuwa lazima watu wakome kuwabagua wanaofanya biashara ya ngono, kwani ni kazi kama kazi nyingine tu.
Wengi walilalamika kuwa jamii imepuuza watu wanaofanya biashara ya ngono wala haiwatetei wakati wanaponyanyaswa au kuuawa .
Ripoyi iliyotolewa mwaka jana kuhusu makahaba mjini Nairobi ilisema
kuwa wanahangaiswa sana na askari wa baraza la jiji na kuwa wengi wao
huachiliwa tu pindi wanapotoa rushwa.
-
-CREDIT:babukubwa magazine