Spika wa Bunge,Anne Makinda.
Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), ameitaka serikali ieleze
kwa nini wananchi watozwe kodi na kampuni za simu bila wenyewe kujua.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Haji aliomba mwongozo wa
Spika kupata maelezo kufuatia kauli ya Naibu Waziri wa Fedha, Janeth
Mbene, kuwa zipo kampuni za simu za mikononi ambazo huwatoza wananchi
kodi nyingine bila wenyewe kufahamu.
Katika swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Ritha
Kabati (CCM), kuhusu kodi zinazotozwa na kampuni ya simu, Naibu Waziri
Mbene alisema zipo nyingi na hata nyingine zinatozwa bila wananchi
kujua.
Hata hivyo, Spika Anne Makinda, alimtaka mbunge huyo kama ana shaka
au hajaridhika na majibu ya waziri, amwandikie barua Spika kupata
maelezo ya ziada.
Katika swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Tauda
Gallos (CCM), alitaka kujua ni kodi gani mpya zimependekezwa kwa mwaka
huu wa fedha na kiasi gani cha mapato ya ziada kimetolewa kukusanywa.
Akijibu, Naibu Waziri alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/14,
serikali imeanzisha kodi ya Sh. 50 kwa lita kwenye mafuta ya petroli na
dizeli kugharimia kusambaza umeme vijijini na kuanzisha kodi ya zuio ya
asilimia tano kwenye huduma za ushauri.
CHANZO: NIPASHE