Na Daniel Mjema
Dodoma.Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda amevunja ukimya na kusema yuko tayari kuachia ngazi
endapo tu Rais Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa na kama itatokea hivyo,
atamshukuru Rais kwa kumwambia, ahsante.
Pinda
aliliambia Bunge mjini Dodoma jana kwamba endapo Rais hatafanya hivyo,
bado wabunge wanayo mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa kwa njia ya
kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Ibara ya
53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge
linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu
endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu,
Rukia Kasim Ahmed (CUF) katika utaratibu wa Bunge wa Waziri Mkuu kujibu
maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge.
Katika
swali lake, Mbunge huyo alisema; Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
alikaririwa akiwa jijini Mbeya kuwa wapo mawaziri mzigo katika Baraza la
Mawaziri.
Mbunge
huyo alisema, katika ziara hiyo, Kinana alifuatana na Katibu wa Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Mahusiano ya
Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro.
"Walipokuwa
Mbeya wakifuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM, Kinana alisema kuna
baadhi ya mawaziri ni mzigo, wewe kama kiongozi mkuu wa shughuli za
Serikali unachukuliaje kauli hii?" aliuliza.
Akijibu
swali hilo, Pinda alisema hata yeye ameyasikia hayo kwenye vyombo vya
habari na kusema, kiutu uzima hawezi kutoa maoni yake kwa kuzingatia
yale yanayosemwa kwenye magazeti.
"Sisi
tunangoja arudi (Kinana) tukae naye ili tujue alichokuwa anasema hasa ni
nini na ninaamini alikuwa na baadhi ya wizara kichwani kwake," alisema
Pinda bungeni jana.
Katika
swali lake la nyongeza, Rukia alisema wakati wanachangia taarifa ya
Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, yupo Mbunge wa CCM alisema kuwa
Pinda ni mzigo namba moja.
"Kuna
mbunge, tena wa CCM, alinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa CCM na akasema
kama ni mawaziri mzigo basi mzigo nambari moja ni wewe Waziri Mkuu,
unawaambiaje Watanzania?" aliuliza Rukia.
Akijibu
swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20 hivyo kama wapo
watakaomhukumu kwa wizara moja ama mbili kwa kutofanya vizuri basi watu
hao watakuwa hawamtendei haki
Kauli ya
Pinda ameitoa siku moja tu baada Bunge kupitisha azimio la kumtaka
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia kupima kama
bado anatosha kuiongoza wizara hiyo.
Pia,
azimio hilo liliwahusu Naibu Mawaziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri na
Kassim Majaliwa kutokana na tuhuma mbalimbali za ufisadi, ubadhirifu na
kuwapo mtandao wa kifisadi ndani ya Tamisemi.
Hata
hivyo, alipohojiwa jana, Ghasia alisema kuwa hana kinyongo na amelipokea
azimio la Bunge. "Sina kinyongo, nimelipokea na ninalitafakari azimio,"
alisema kwa kifupi.
Naye
Mwanri alisema kuwa hakuwa na habari kama suala la Tamisemi linamuhusu
na yeye na kwamba atakapothibitika kuwa ni miongoni mwao, ndipo atakuwa
kwenye nafasi ya kujibu.
Tangu
kuanza kwa mkutano wa 14 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, kumekuwapo
vuguvugu la kuwang'oa mawaziri waliotajwa na Kinana kuwa ni mzigo katika
kutekeleza majukumu yao.
Mbunge wa
Mwibara, Kangi Lugola (CCM), yeye alienda mbali na kumshauri Rais
kumfukuza kazi Pinda kutokana na kuwa mpole mno kiasi kwamba mawaziri
wanamdharau na hawamsikilizi.
Pendekezo
hilo liliungwa mkono pia na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR-Mageuzi) na wabunge wengine waliochangia taarifa za Kamati za
Bunge walionyesha shaka dhidi ya Pinda.
Ghasia afunguka
Ghasia,
ambaye yeye na wasaidizi wake waliundiwa Azimio la Bunge kujipima juzi,
amefunguka na kusema analifanyia kazi azimio hilo kabla ya kuchukua
uamuzi wa kufanya chochote.
Juzi
Bunge lilipitisha azimio la pamoja kuwataka Waziri na Naibu Mawaziri
katika Wizara ya Tamisemi kujitathmini wenyewe kabla ya kufikia uamuzi
kutokana na kuelezwa kuwa wameshindwa kusimamia majukumu yao.
Azimio la
wabunge lilipitishwa na wabunge kwa kura ya 'ndiyo' bila ya kupingwa
baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda iwapo wabunge
wanaipokea Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(Laac) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Rajab Mbarouk.
"Mimi
nimepokea Azimio hilo bila shaka siwezi kusema chochote kwa sasa kwani
naendelea kulifanyia kazi baada ya hapo nitakuwa na cha kusema,
nashukuru kwa kuniuliza," alisema Waziri Ghasia kwa njia ya simu
Kwa
upande wake, Mwanri alisema yeye si mlengwa katika jambo hilo hivyo
hawezi kusema chochote. Alisema Azimio hilo lilimgusa moja kwa moja
Waziri wa Tamisemi ambaye si yeye hivyo kutoa majibu ya jambo hilo si
wakati wake.
"Mimi
nilivyosikia na nilivyoelewa ni waziri mwenyewe ndiye anayeguswa moja
kwa moja na jambo hilo, kwa hiyo unaweza kwenda kwake atakuwa na majibu
ya kukupa na bila shaka atakusaidia vizuri," alisisitiza Mwanri.
Kwa upande wake Kassim Majaliwa hakupatikana kuzungumzia jambo hilo kwa madai kuwa yuko nje ya nchi kwa shughuli za kiserikali.
MWANANCHI