TAARIFA YA AJALI YA MOTO KATIKA OFISI ZA CHADEMA MKOANI ARUSHA

Ofisi za Chadema zilizoungua kwa moto Arusha.
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
                                                                         
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA OFISI YA KAMANDA WA POLISI MKOA WA ARUSHA: TAARIFA YA AJALI YA MOTO KATIKA OFISI ZA CHADEMA
Ndugu wanahabari, mnamo tarehe 03/12/2013 muda wa saa 5:00 asubuhi, polisi mkoani hapa tulipokea taarifa juu ya kuchomwa moto kwa jengo ambalo lina ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zilizopo mtaa wa Ngarenaro, Halmashauri ya jiji la Arusha.
Mara baada ya taarifa hiyo askari walikwenda katika eneo la tukio na kukuta moto umezimika. Jengo hilo ambalo lina uzio mrefu wa matofali na geti moja la mbele lina ofisi tatu za chama hicho ambazo ni ofisi za wilaya, mkoa na Kanda ya Kaskazini ambazo zinatumia bafu na choo kimoja.
Aidha uchunguzi uliofanywa na polisi kwa kushirikiana na idara ya zimamoto imegundua mambo yafuatayo:-
  • Kwanza, ofisi hizo zinalindwa na walinzi wa chama hicho “red brigades” na siku ya tukio mlinzi aliyekuwa zamu alikuwa Kitumbwizi s/o Bahati (42) mkazi wa Olasiti ambaye aliingia kazini tarehe 02/12/2013 muda wa saa 12:00 jioni na kutoka tarehe 03/12/2013 muda wa saa 12:00 asubuhi. Aidha ofisi hizo zina katibu muhtasi mmoja aitwaye Jenifer d/o Mwasha (25) mkazi wa Sombetini ambaye uwa anaingia kazini saa 1:30 asubuhi kila siku lakini siku ya tukio aliingia saa 4:00 asubuhi.
  • Pili, uchunguzi umeendelea kubaini kuwa, hakuna mahali palipovunjwa kutoka kwenye uzio wa ofisi hizo kuruhusu mtu/watu kuingia ndani.
  • Tatu, mlango wa nyuma wa ofisi hizo katika veranda kuligundulika tundu katika dari kuelekea bafuni tundu lenye upana wa futi moja na nusu kwa nusu (11/2x1/2) ambalo ni dogo kiasi cha kutowezesha mtu kupenya kuingia ndani ya ofisi hizo.
  • Nne, ndani ya bafu kulipatikana majivu na kwenye sakafu na juu ya sinki yakiwa makavu bila maji maji yoyote.
  • Tano, kuta zote za bafu na choo hazikuwa zimeungua.
  • Sita, eneo lililoungua kwenye dari ni 3/4 (robo tatu mita) lenye upana wa mita 1 kwa urefu wa mita 3.
  • Saba, eneo ambalo moto ulionekana umewaka, mbao katika dari zilionekana kuungua upande wa chini na upande wa juu wa mbao na ceiling board hazijaungua kuomyesha moto ulianzia chini.
  • Nane, kumepatikana kipande cha chuma kilichokuwa na karatasi zilizoungua pamoja na tochi ndani ya dari eneo ambalo moto ulikuwa ukiwaka lakini vitu hivyo havikuonyesha dalili za kuungua au kushika moto, na inaonyesha vimewekwa baada ya moto kuzimwa.
  • Tisa, kuna uwezekano mkubwa moto huo ulizimwa kwa kutumia hewa chafu/co2.
Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi bado linaendelea kuwahoji mlinzi wa ofisi hizo Kitumbwizi s/o Bahati pamoja na Katibu muhtasi Jenifer d/o Mwasha, huku upelelezi zaidi juu ya tukio hilo ukiendelea.
 
Asanteni kwa kunisikiliza.
IMETOLEWA NA KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA ARUSHA,
KAMISHNA MSAIDIZI WA POLISI (ACP) JAPHET LUSINGU
TAREHE 04/12/2013.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...