WAISLAMU WATAKIWA KUTOLALAMIKIA WAKRISTO

 
Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba.
SHEKHE Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba, ametaka Waislamu kuacha kulalamika, kwamba Wakristo wamekuwa wakipewa upendeleo, badala yake watumie fursa wanazopata kuondokana na malalamiko hayo. Akizungumza katika maadhimisho ya Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma jana, Mufti Simba alisema chanzo cha malalamiko hayo ni Waislamu kushindwa kujitolea katika mambo mbalimbali ya maendeleo.
Akitoa mfano, alisema Waislamu wanapaswa kupeleka watoto wao kusoma elimu zote mbili na kuwaandaa kushika nafasi za kiutendaji ambazo wanalalamikia kuwa zimetolewa kwa upendeleo kwa Wakristo.
Alisema hata katika kukamata maeneo ya uwekezaji, Waislamu wamebaki nyuma kutokana na kushindwa kujitolea kuchangia fedha za kutosha za kuanzisha miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuimarisha dini na kuendesha maisha yao.
“Msilalamike, tunisheni mifuko katika misikitini yenu muwe na fedha za kutosha zitakazokuwa kichocheo cha ninyi kushiriki katika shughuli muhimu za kiuchumi. Kosa ni lenu, msilalamikie Wakristo hawana tatizo hata kidogo katika hilo,” alisema Mufti Simba.
Madaraka misikitini Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Taifa, Ally Mkoyogore, alitaka Waislamu kuongeza bidii katika elimu na uchumi, badala ya kutumia muda mwingi kupigania madaraka misikitini.
Alisema kurudi nyuma kwa Waislamu, kunasababishwa nao wenyewe kushindwa kufuata maadili na misingi ya dini yao, badala yake wanagombea uongozi misikitini kwa ajili ya maslahi binafsi.
Maadhimisho hayo ya Maulid yalihudhuriwa na viongozi wa dini kutoka mikoa mbalimbali nchini, mashekhe kutoka Burundi huku Serikali ikiwakilishwa na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya.
Mshikamano Akizungumza katika mkesha wa Maulid usiku wa kuamkia jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Rais mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alitaka Watanzania kujenga mshikamano kwa kusikilizana na kuvumiliana, kwa lengo la kudumisha tunu ya amani na utulivu iliyodumu kwa miaka mingi sasa nchini.
Katika salamu zake za siku hiyo, Alhaji Mwinyi alisema dini zote ukiwamo Uislamu, hazikatazi waumini kushirikiana katika masuala mbalimbali, hivyo ni wajibu wa kila upande kuusikiliza mwingine.
“Nchi zinaijua Tanzania kuwa kisiwa cha amani kisicho na utofauti wa dini, kabila wala rangi. Sote ni ndugu wamoja, tunapaswa kuendelea kuishi kwa usalama na amani.
“Pale inapotokea hali ya kutofautiana, tukae pamoja na kuzungumza ili tufikie mwafaka na si kugombana,” alisema Mwinyi.
Alisema Mtume aliongoza dini kwa kuhubiri mshikamano, kupenda wengine na kuthamini utu na si vurugu kama ambavyo wengine wanadhani.
Akimkaribisha Mwinyi kutoa salamu hizo, Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salumu, alisema amani na utulivu nchini ndio ujumbe wa sherehe hizo na kukumbusha Watanzania kuishi kwa umoja na kuwa watu wa Taifa moja lisilo na uvunjifu wa amani.
Kutokana na umuhimu huo, Shekhe Alhad alisema ndiyo maana sherehe hizo zikapewa kaulimbiu ya ‘Uislamu ni amani kwa wote’ lengo likiwa kukumbusha wanaofikiri kuwa misingi ya dini hiyo ni vurugu na kuhatarisha usalama au kujenga uadui kwa watu wengine.
Katiba mpya Shekhe Alhad pia alimpongeza tena Rais Kikwete kwa kufanikisha kwa kiasi kikubwa mchakato wa Katiba mpya ambao hivi karibuni utaingia katika hatua ya uundwaji wa Bunge Maalumu.
“Kama ni safari basi tayari mchakato wa Katiba umevuka Nungwi na karibu unaingia bandarini. Ni jambo la kumpongeza kwa sababu si mataifa yote yangeweza kufika hadi hapa tulipo bila vurugu, ila sisi tumeweza na hata pale palipotokea changamoto fulani, alikabiliana nazo,” alisema Shekhe Salum.
Alisema ni vema Watanzania wazidi kumwombea kiongozi huyo ili akamilishe salama mchakato huo na kumalizia muda wa uongozi na kumkabidhi mtu mwingine kuongoza Taifa. Miongoni mwa wageni waliokuwepo ni Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Imeandikwa na Fadhili Abdallah, Kigoma na Oscar Job, Dar
CHANZO NI HABARI LEO


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...