Operesheni
ya kusafisha jiji ili kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (wamachinga)
kwenye maeneo yasiyo rasmi, imewageukia watoto wanaoishi kwenye
mazingira magumu na ombaomba.Operesheni hiyo inaendeshwa na Halmashauri
ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Akizungumza,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema uongozi
wa Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendesha
operesheni hiyo kwa ajili ya mkazi wa wilaya hiyo kufanya kazi zake kwa
kufuata sheria. (J.G)
Alisema
hatua ya kuwaondoa watoto hao na ombaomba imetokana na ongezeko la watu
hao, ambao wengi wao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo huku wakiwa
wanajiweza kifamilia.
"Sisi ni
wasimamizi wa operesheni hiyo, wahusika wakuu ni halmashauri. Hata
hivyo, wanapowaondoa mitaani yapo maeneo ya kuwahifadhi," alisema
Minangi.
Alisema
operesheni hiyo ya safisha jiji kwa utaratibu ulivyopangwa ni kwamba
haitabakiza chochote na kusema kuwa kila anayejijua kuwa anakiuka sheria
ni vema akajiepusha na vitendo hivyo kabla ya kufikiwa na mkono wa
sheria.
Kamanda Minangi alisema operesheni hiyo inakwenda sambamba na zuio la pikipiki, bajaji na guta kuingia katikati ya jiji.
Jiji la Dar
es Salaam sasa linaonekana kuwa safi ikiwemo hifadhi ya barabara kurudi
kwenye hali ya kawaida na kuondoa msongamano, kutokana na operesheni
hiyo iliyoanza siku mbili zilizopita.