MAPENZI ya jinsia moja ni moja ya
biashara inayozidi kushamiri katika nchi za Afrika Mashariki na
kuchangia maambukizi makubwa ya Ukimwi. Kutokana na hali hiyo, nchi za
Afrika Mashariki zimetakiwa kuangalia namna ya kuokoa maisha ya mashoga,
ili wasiendelee kuteketea na ugonjwa hatari wa Ukimwi badala ya
kuwanyanyapaa.
Akizungumza jana katika mkutano
unaojadili masuala ya afya kwa watu wanaosafiri, wahamiaji na watu
wanaozunguka sehemu mbalimbali, Mratibu wa Chama cha Watu wanaofanya
biashara ya ngono nchini Kenya, John Mathenge alisema jambo la hatari ni
kwamba hata viongozi wakubwa serikalini wanapenda kufanya mapenzi na
mashoga.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Asasi
ya Kimataifa ya Wahamiaji (IOM), Mathenge alisema pamoja na desturi za
kiafrika kukataza vitendo vya ushoga na usagaji, lakini wapo watu katika
jamii wanaofanya mapenzi hayo kama biashara ya kuwapatia kipato au
kujifurahisha.
Alisema shirikisho la watu wanaofanya kazi za mapenzi lina wanachama wengi hapa nchini wapatao kama 40,000.
"Unajua biashara hii ya kuuza mwili ni
kazi sawa na kazi zingine, mtu anaweza kuamua atumie mwili wake kuwa
mkimbiaji, mwingine kuwa kahaba au shoga zote hizi ni kazi na wanaofanya
kazi hiyo hawapaswi kulaumiwa na jamii bali wasaidiwe ili wasiambukizwe
Ukimwi," alisema.
Alisema kwa kuwa watu hao wako katika
jamii yetu na wanafanya mapenzi na viongozi na watu wa kawaida,
maambukizi ya Ukimwi yanazidi kuongezeka hivyo kuna haja ya Serikali
kukubali kuzungumza na mashoga na makahaba wengine ili kuangalia namna
ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
"Tuache tabia ya kuwanyanyapaa, tukienda
hospitali tunanyanyapaliwa tunaambiwa twende na wapenzi wetu, tutawatoa
wapi wakati mtu umekutana naye kwa siku moja tu? Ukweli ni kwamba kila
mtu hapa duniani anafanya biashara ya ngono ila katika mfumo tofauti.
"Wewe wakati unataka kuoa mke wako
ulitoa mahari ili aje kwako, au kuna watu wana vimada wanawapelekea
zawadi ili waendelee kupewa mapenzi, hawa nao wanafanya biashara ya
ngono, sasa iweje sisi ambao tumejitokeza tuanze kunyanyapaliwa? Alihoji
Mathenge.
Alisema hata kuongezeka kwa wahamiaji
haramu kumetokana na kuwepo biashara hiyo ya ngono ambayo inafanywa na
maofisa wa Serikali kama Uhamiaji ambao wanapewa ngono na wasichana na
kuwaachia waingie kwenye nchi husika bila kuwa na vibali vinavyotakiwa
kisheria.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Madereva Mohamed Sharrif Abdukadir, alisema urasimu uliopo kwenye mipaka
katika kushughulikia nyaraka za mizigo ndizo zimekuwa zinachangia
madereva wanaosafiri kwenda nchi jirani kuingia katika vitendo vya
ngono.
Alitoa mfano wa mpaka wa Tunduma kuwa
unaongoza kwa kuwa na urasimu kutokana na mfumo uliopo wa kushughulikia
nyaraka hali inayomfanya dereva wakati mwingine akae wiki mbili eneo
hilo hivyo kujikuta anafanya vitendo vya ngono.
Hata hivyo alisema asasi ya IOM kwa
kushirikiana na Chama cha Madereva wa Masafa Marefu imewasaidia kuwapa
ushauri wa namna ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi wakati wanapokuwa
safarini.
Abdukadir alisema tayari kumejengwa
vituo vijulikanavyo kama One Stop Border Posts ambavyo vinatumiwa na
madereva kwenda kupata ushauri na kupima afya zao.
Alisema vituo hivyo viko chini ya IOM
vinatoa semina kwa madereva na hata kama mtu anakutwa ameambukizwa
anapewa dawa za kurefusha maisha. Eva Mwai ambaye ni Mratibu wa Asasi ya
North Star Alliance katika ukanda wa Afrika Mashariki, anasema asasi
yake imekuwa inatoa msaada wa kiafya kwa watu wanaozunguka kwa vile
hawana muda wa kwenda kupimwa hospitalini.
Alisema wanafanya utafiti katika maeneo
mbalimbali ambako ni hatarishi kwa madereva na wanajenga kliniki maalumu
kwa ajili ya kutoa afya na ushauri kwa madereva na watu wengine ambao
wana maisha ya kuzunguka.
Alisema wana vituo vya afya huko Mombasa, Tunduma, Kahama na Mwanza kwa ajili ya kufanya upimaji kwa watu wanaozunguka.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi Mbarak Abdulwakil aliwataka washiriki wa mkutano huo ambao wanatoka
nchi mbalimbali kubadilisha uzoefu wa namna ya kushughulikia afya kwa
watu wanaozunguka, wahamiaji mbalimbali hasa katika eneo hili la ukanda
wa Afrika Mashariki