Marehemu Lesego Motsepe ‘Lettie Matabane’ enzi za uhai wake.
Sifael Paul na Mtandao
KIFO cha staa aliyekuwa mwingizaji wa shoo ya runingani ya Isidingo ‘The Need’, Lesego Motsepe ‘Lettie Matabane’ kimeibua vilio kwa ‘Wasauzi’ ikielezwa chanzo ni ugonjwa hatari wa Ukimwi, huu ndiyo undani kamili.
Lettie Matabane aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 40, alikutwa na kaka yake, Moemise Motsepe akiwa amefariki dunia nyumbani kwake Randburg, Gauteng jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Jumatatu wiki hii kisha mwili wake kuhifadhiwa hospitalini kwa mazishi.
Kwa mujibu wa kaka yake huyo, mwigizaji huyo aliyekuwa na kipaji kikubwa cha uigizaji, uimbaji, uprodyuza na uandishi wa stori za sinema alikufa kifo cha taratibu akiwa usingizini.
Desemba mwaka 2011, Lettie alionekana amedhoofu wakati akitangaza kuwa alikuwa muathirika wa Virusi vya Ukimwi kupitia Redio Kaya FM ya Afrika Kusini, ikiwa ni sehemu ya tahadhari juu ya ugonjwa huo.
Ilikuwa Desemba Mosi, 2011, Siku ya Ukimwi Duniani. Alitangaza kuwa aliishi na virusi hivyo tangu mwaka 1998, miaka 16 kabla ya kifo chake.
Alianza kutumia vidonge vya kurefusha muda na kupunguza makali ya virusi, ARVs tangu mwaka 2010.
Mwaka 2012, Lettie ambaye hakuwa na mume alitangaza kupitia 3Talk ya Runinga ya SABC3 kuwa aliacha kutumia ARVs na kuamua kutumia njia ya asili kama matibabu.
Alidai matibabu hayo yatajumuisha tafakuri yakinifu (meditation) na kufuata ‘dayati’.
Kabla ya umauti, Lettie Matabane alikuwa mwanaharakati wa kupinga maambukizi ya VVU kwa miaka mingi kupitia shirika la kijamii la kusaidia vijana la Afrikarize.
Familia yake na jamii iliyomzunguka ilimtumia kama mzungumzaji wa kuhamasisha (motivational speaker) kabla ya kukutwa na maradhi hayo.
Kwa mujibu wa mashabiki wake, Lettie Matabane hakuwa msiri, alipenda mambo yake hata yale ya binafsi yawe wazi ndiyo maana hakuficha suala la VVU.
“Wakati tukiomboleza kifo cha mwanamke mzuri (Lettie) pia tusherekee maisha na matumaini aliyotuachia ambayo yanasaidia vijana duniani kote,” walisema baadhi ya Wasauzi waliokuwa wakimlilia Lettie Matabane katika mitaa mbalimbali ya Johannesburg na kuongeza:
“Lettie alikuwa na kipaji cha kipekee, ni vizuri tukakienzi kama sehemu ya kumbukumbu ya burudani aliyotupatia kupitia Isidingo. Ni huzuni kwa tasnia ya uigizaji duniani kote.”
Katika kipindi chote cha mateso ya kuumwa kwake, Lettie Matabane alikuwa akisaidiwa na mama yake, Ivy Skhosana na kaka zake wawili, Andile Skosana na Moemise Motsepe.
Katika Isidingo ambako alionekana kwa zaidi ya miaka 10 huku Wabongo wakifuatilia kupitia Runinga ya ITV, Lettie Matabane alisota na mama yake (wa kwenye Tamthiliya) hadi alipofariki dunia kwa ajali. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuonekana kwa Lettie Matabane kwenye Isidingo.
Baadhi ya mastaa wa Isidingo walimpongeza kwa kitendo chake cha kuwa muwazi juu ya VVU kwani alifanikiwa kupiga vita juu ya maambukizi mapya.