Media For Development International (MFDI) – Tanzania
usiku wa jana wamefanya uzinduzi wa aina yake katika sekta ya filamu
Tanzania kwa kuzindua filamu tatu kupitia mradi wake wa Swahiliwood
katika Ukumbi wa Century Cinemax uliopo Oysterbay, jijini Dar es salaam.
Uzinduzi
huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya filamu hapa nchini
pamoja na mashirika ya ya ndani na nje ya nchi ikiwa ni hatua ya kuleta
mapinduzi makubwa katika sekta ya filamu hapa nchini.
Filamu zilizozinduliwa jana zikiwa na lengo la kuelimisha jamii ni Mdundiko iliyotengenezwa na Timothy Conrad, Sunshine iliyotengenezwa na Karabani na Network iliyotengenezwa na John Kallage.
Mradi wa Swahiliwood umewezeshwa kwa msaada wa Watu wa Marekani kupitia USAID kwa kushirikiana na Johns Hopkins University
Center for Communication Programs pamoja na kampuni ya Proin Promotion
inayokuwa kwa kasi katika usambazaji wa kazi za filamu nchini Tanzania.
Lengo la
Swahiliwood ni kuongeza nguvu ya ubunifu kwa vijana watengeneza filamu
wa Kitanzania, ili kupeleka maudhui kwa walengwa kwa njia ya burudani
kwa kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha filamu zinawafikia
walengwa mbalimbali kupitia mitandao ya wasambazaji. Mradi huu unafanya
kazi pamoja kwa kushirikiana na wadau muhimu kutoka sekta ya umma pamoja
na COSOTA (Chama cha haki miliki), Mamlaka ya mapato Tanzania, bodi ya
filamu na BASATA, kama idara inayosimamia maendeleo ya Tasnia vya
filamu.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi John Riber, mkurugenzi MFDI Tanzania alisema kwamba
“Tulizindua mradi wa Swahiliwood kwa sababu tuliona kwamba vijana wana
uwezo mkubwa wa kutengeneza filamu. Muundo wa Swahiliwood unazingatia
nguvu ya vijana katika kuhakikisha tasnia ya filamu inasambaa
ikielimisha jamii juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Na hiyo
imetambuliwa na Serikali ya Tanzania kama ni changamoto kuu ambayo
inalikabili Taifa”.
Muundo wa
Swahiliwood unatoa mafunzo na ushauri kwenye uzalishaji wa filamu. Pia
ni sekta ambayo inaongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania.
Serikali ya Tanzania na sekta binafsi pamoja na Watanzania wabunifu
wenye vipaji vya utengenezaji wa filamu wameshirikiana, kwa msaada wa
Serikali ya Marekani. Wamekuwa nyenzo katika kukuza biashara na uchumi
unaokuwa haraka, na kuhakikisha kwamba filamu zinawafikia watazamaji wa Afrika ya Mashariki kwa ujumla.
MDUNDIKO: Ni hadithi ambayo inazungumzia mfarakano wa imani za kimila, maadili, na hoja za maisha katika jamii. NETWORK:
Ni hadithi inayohusu kuwindwa kwa mhalifu anae tuhumiwa kufanya mauaji
ya mwendelezo ambayo yanawahusisha wapelelezi, askari mzee na kijana
mwenye mvuto.
SUNSHINE: Ni hadithi ya uraiani yenye mguso kuhusu majaribu ya uhalifu na mapenzi yasiyokuwa na mashariti kati ya mama na mtoto.