MBUNGE wa Bahi kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Omar Baduel amesema hatajiuzulu kwenye nafasi hiyo,
kutokana na kuandamwa na baadhi ya madiwani kwa tuhuma za kutumia vibaya
fedha za mfuko wa jimbo. Alitoa kauli hiyo juzi kwenye kikao cha baraza
la madiwani la halmashauri ya Bahi.
Alisema hayo baada ya kamati iliyoundwa
kuchunguza tuhuma dhidi yake, kutoa taarifa na kuonesha Mbunge huyo
alitumia kwa maslahi yake fedha za Mfuko wa Jimbo, ambao hutolewa kwa
ajili ya shughuli za maendeleo.
“Sio kweli hayo yaliyoandikwa kwenye
taarifa, niliitwa kwenye tume, niliyosema humo hayamo, mnyonge mnyongeni
lakini haki yake mpeni,” alisema.
Alisema hiyo si mara ya kwanza kuandamwa
na baraza hilo la madiwani, kwani hata alipokuwa Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, ilikuwa hivyo, hali iliyosababisha ajiuzulu nafasi
hiyo, lakini alipoamua kugombea Ubunge alipata.
“Hamnitendei haki, nimesikitishwa na
taarifa hiyo yenye nia ya kufanya nitoke kwenye ubunge, ila namshukuru
Mwenyezi Mungu sina sauti ninaposhambuliwa na kundi la watu,” alisema
Mbunge huyo. Alisema hawezi kubadilisha makusudio na nia ya watu, ambao
wamekuwa wakimuandama mara kwa mara.
“Safari hii sijiuzulu, kuna watu wanaota Ubunge humu,” alisema.
Akisoma taarifa ya tume hiyo, Mwenyekiti
wa Kamati ya Uhakiki Fedha za Mfuko wa Jimbo, Julius Chitojo alisema
baraza la madiwani lililoketi Oktoba 31, mwaka jana, lilipokea hoja
binafsi kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Mfuko wa Jimbo.
Alisema baraza liliazimia kuunda kamati
ya watu wanne ili kufuatilia na kubaini ukweli wa hoja, zilizotolewa na
Diwani wa Lamaiti, Donald Mejitii kuwa mbunge huyo alifanya ubadhirifu
wa fedha zilizotolewa kwa vikundi, ununuzi na usambazaji wa majembe ya
kukokotwa na ng’ombe hasa katika kipindi cha kuanzia Agosti mwaka jana.
Pia alisema michango ya fedha za wananchi
wa kijiji cha Chibelela kwa ajili ya kusafisha kisima cha maji
zilichukuliwa na mbunge huyo, lakini hazikutumika kwa kazi iliyopangwa.
Mwenyekiti huyo alisema kikao cha kamati
ya maendeleo ya Mfuko wa Jimbo, kilichofanyika Aprili 30, mwaka jana
kiliidhinisha Sh milioni 17 kwa ajili ya ununuzi wa majembe 117 na Sh
milioni 3.2 kwa ajili ya usafirishaji wa majembe hadi kwa walengwa.
Hata hivyo, alisema hadi kufikia Oktoba
30, mwaka jana, majembe yaliyosambazwa yalikuwa ni 85 yenye thamani ya
Sh milioni 14.5, kati ya hayo majembe 78 yaliuzwa kwa Sh 110,000 kila
moja sawa na Sh milioni 8.5.
Taarifa hiyo ilisema fedha nyingine za
uuzaji wa majembe hayo, zilikuwa zikikusanywa na Msaidizi wa Mbunge
huyo, Saidi Kayumbo ambaye baada ya kuhojiwa na kamati, alisema fedha
hizo alikuwa akipeleka kwa mbunge huyo, badala ya fedha hizo kupelekwa
halmashauri.
Pia, mbunge huyo alikuwa akivitaka
vikundi kutumia akaunti ya Jumuiya ya Akiba na Maendeleo Bahi (BASATA)
ili fedha zao za maendeleo ya ziingie humo, licha ya kuwa vikundi
husika, vilikuwa na akaunti za benki.
Alisema kutokana na kubaini hayo, baraza
lichukue hatua stahiki kwa mbunge huyo pamoja na kurejesha fedha zote
alizochukua, ambazo zilitengwa kwa shughuli za maendeleo.
Diwani wa Lamaiti, Donald Mejitii alidai
mbunge huyo alikuwa akitumia gari lake kusambaza pembejeo hizo huku
akiwadai wananchi fedha za usafiri.