Dar es Salaam. Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imesema watu 15 waliokamatwa na dawa
za kulevya nchini China, hawatanyongwa na badala yake watafungwa maisha
nchini humo kutokana na mawasiliano mazuri ya kidiplomasia baina ya
Tanzania na China.
Kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo mtu yoyote anayekamatwa na dawa za kulevya adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari juu ya
mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya watu wa China nchini mwaka
jana, Xi jinping, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, John Haule alisema nchi
hizo mbili zina uhusiano wa muda mrefu na wa kidugu katika nyanja za
siasa, uchumi, usalama na jamii.
Haule alisema kutokana na uhusiano mzuri kwa nchi
hizo mbili kwa kushirikiana mambo mbalimbali, hivyo wafungwa
waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa hawatanyongwa na badala yake
watafungwa maisha.
“Tunaushirikiano mkubwa sana ndiyo maana
Watanzania waliohukumiwa kunyongwa sasa hivi hawatanyongwa tena na
badala yake watatumikia kifungo cha maisha gerezani,” alisema.
Haule alisema mwaka huu nchi hizo mbili
zinajivunia kuadhimisha miaka 50 ya uhusiano ya kidiplomasia ambayo
imekuwa na mafanikio katika nyanja mbalimbali.
Alisema kupitia ziara ya Rais Xi Jinping alipata
fursa ya kutangaza sera mbalimbali na utayari wa kushirikiana katika
kukabiliana na changamoto za kimaendeleo zinazotokea duniani kote.
“Ikumbukwe kwamba, moja ya vielelezo vikubwa
kabisa vya ushirikiano wa nchi hizi mbili ni Reli ya Tazara (Reli ya
Tanzania na Zambia), Kiwanda cha Nguo cha Urafiki na kwa wale wapenzi wa
Soka, Uwanja wa Kisasa wa Mpira wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000
wakiwa wamekaa,” alisema Haule.