Halmashauri pamoja na wadau toka mashirika
na taasisi za kutetea na kulinda haki za watoto jijini Mwanza wameanza
rasmi vikao vya maandalizi ya kuadhimisha sherehe za siku ya mtoto wa
Afrika inayoadhimishwa kila Mwaka Juni 16.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa
Halmashauri wa Jiji la Mwanza chini ya Afisa Maendeleo ya Jamii wa
Halmashauri hiyo Bi. Eluminatha Mwita wajumbe walikubaliana kuadhimisha
siku hiyo katika Kata ya Buhongwa, kwa Wilaya ya Nyamagana.
Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa
kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu, na umuhimu wa
mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanywa kila juni 16 tangu
ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho
Afisa Maendeleo Jamii wa Jiji la Mwanza Bi. Eluminatha Mwita alisema
kuwa kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa
Watoto ni Jukumu Letu Sote” na kufafanua kuwa kauli hiyo inalenga
kuwasisitiza wazazi na walezi kuacha mila potofu zenye kuleta madhara
kwa watoto.
Bi Eluminatha alisema kuwa “Kauli mbiu hiyo
ina lenga kuangalia mila zote kandamizi na potofu zinazotokana na jamii
husika katika malezi ya mtoto na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo
kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kubakwa kwa watoto, kukosa elimu,
afya na malezi bora pamoja na vifo kwa watoto hawa”.
Kikao hicho cha kwanza kiliweza kuchagua
viongozi wa kamati hiyo ya maandalizi, mwenyekiti aliyechaguliwa ni
Godfrey Salum huku katibu ni Devis Mrope na katibu msaidizi akichaguliwa
Francisca Michael, baada ya kupata viongozi kamati nne ziliundwa na
wajumbe, Kamati ya Uratibu, Mipango na Fedha, Kamati ya Usafiri na
Ulinzi, Kamati ya Mapambo na Burudani pamoja na kamati ya Hotuba na
Habari.