SERIKALI YADHAMIRIA KUJENGA RELI MPYA

Waziri wa Uchukuzi,Dk. Harrison Mwakyembe
 
Waziri  wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (pichani), amesema serikali imedhamiria kujenga reli mpya ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kwa ajili ya kusafirisha mizigo mikubwa kutoka Bandarini.
Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete, kufungua mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Kimataifa uliohusisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

"Tulianza kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali na leo hii tunaendelea kama wakitukubalia, tutuanza ujenzi mwaka huu na hili hatutanii kwa sababu hatuna namna mizigo ni mingi bandarini," alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa ina uwezo wa kupokea tani milioni 13, lakini uwezo wa Reli ya Kati kusafirisha mizigo ni tani 200,000 na kwamba tani milioni 12.8 inasafirishwa kupitia njia ya barabara.

Alisema nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea kiuchumi ikiwa itaendelea kusafirisha mizigo mingi kwa kutumia njia ya barabara.

Aliongeza kuwa mizigo mingi ikipitia barabara, ni rahisi kuziharibu. Alisema Tanzania imedhamiria kujenga reli mpya na pana yenye urefu wa kilomita 2,707.

"Kwa kutumia fedha zetu za ndani hatuwezi kujenga reli mpya hata siku moja tutaishia kufanya ukarabati mdogo mdogo ambao tunaendelea nao," alisema Dk. Mwakyembe.
CHANZO: NIPASHE


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...