TRL YASITISHA SAFARI KWA SIKU SABA


  Kilichowakera abiria ni kupewa taarifa hiyo ghafla tena bila kuelezwa sababu ya hatua hiyo. Mzozo huo ulizimwa kwa busara za askari polisi wa reli na wa kampuni binafsi ya ulinzi waliokuwapo katika stesheni hiyo
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), imesitisha safari za treni ya Reli ya kati kwa siku saba kutokana na kubainika hitilafu katika Daraja la Ruvu.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Kipallo Kisamfu alisema: “Itachukua takriban siku saba hivi hivyo kuanzia jana (juzi), eneo la reli lenye urefu wa kilometa 82 kutoka Dar es Salaam hadi Ruvu limesitishwa kwa muda kutoa huduma ya usafiri wa reli.”
Juzi, shirika hilo lilitangaza kusitishwa ghafla kwa safari kutokana na kubainika kuwepo nyufa katika daraja hilo na kuzua vurumai baina ya maofisa wa TRL na abiria.
Kilichowakera abiria ni kupewa taarifa hiyo ghafla tena bila kuelezwa sababu ya hatua hiyo. Mzozo huo ulizimwa kwa busara za askari polisi wa reli na wa kampuni binafsi ya ulinzi waliokuwapo katika stesheni hiyo.
Ofisa Habari wa TRL, Midradjy Maez alisema baadaye kuwa usafiri huo umesitishwa kutokana na kubainika kwa nyufa hizo na timu ya wahandisi wa kampuni hiyo ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji ilikuwa imekwenda eneo la tukio.
 Chanzo:Mwananchi


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...