SIKU moja baada ya Mbunge wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, Bw. John Shibuda kutangaza kuachia ngazi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mbunge huyo ameibuka tena na kusema aliahidiwa kupewa helikopta mbili na uongozi wa chama hicho aweze kuzitumia katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010 lakini hakupewa.
Alisema
uongozi wa chama hicho ukiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Wilbrod Slaa,
ulimwahidi kumpa helikopta hizo kwenye kampeni zake na kumpigia debe
Katibu huyo aliyekuwa akiwania nafasi ya urais.
Bw.
Shibuda aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Kata ya Malampaka, wilayani Maswa na kuongeza kuwa, alijitolea
kutumia pesa zake katika uchaguzi huo na kuahidiwa kurudishiwa lakini
mpaka sasa bado kurudishwa.
“Katika
kampeni za mwaka 2010, mbali ya kuahidiwa helikopta, pia nilikuwa
chanzo kikubwa cha Dkt. Slaa kupata kura nyingi kwa mara ya kwanza na
kuongoza kwenye Wilaya ya Maswa akimzidi mgombea mwenzake kutoka CCM,
Rais Jakaya Kikwete.
“Helikopta
nilizoahidiwa, hata wakati wa kampeni sikupewa, nilipouliza niliambiwa
nitapewa…mimi ndiye chanzo kikubwa cha Rais Kikwete kupata kura ndogo
katika jimbo langu, nilitumia gharama zangu kumfanyia kampeni Dkt.
Slaa,” alisema.
Wakati
huo huo, Bw. Shibuda alisema msimamo wake ni Serikali mbili na
kusisitiza hawezi kuwaunga mkono wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao msimamo wao ni Serikali
tatu ambazo zitawaongezea mzigo wananchi wangu ambao ni wakulima na
wafugaji.
Bw.
Shibuda alisema wananchi wake hawataki kuongezewa mzigo wa Serikali;
bali wanataka kutatuliwa kero walizonazo hasa zinazohusu kilimo cha
pamba, migogoro ya wakulima na wafugaji.
“Siko
tayari kuunga mkono muundo wa Serikali tatu kwa sababu wakulima wa
pamba wana matatizo makubwa katika bei ya zao hili na pembejeo, pia
katika wilaya yangu kuna migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji
inayopaswa kutatuliwa kwa serikali hii tuliyonayo,” alisema Bw. Shibuda.
Katika
mkutano huo, Bw. Shibuda alikwenda mbali zaidi akimfananisha Mbunge wa
Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria wa chama hicho, Bw. Tundu
Lissu na kundi la Interahamwe lililochochea ubaguzi wa kikabila
uliosababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda akidai mbunge huyo amekuwa
mchochezi wa vita ndani na nje ya chama.
“Tundu
Lissu ni Interahamwe kwani amekuwa mtu mchochezi mwenye tabia ya
kuwatukana wenzake, hana tofauti na kundi hili kama wenzake
walivyosababisha mauaji nchini Rwanda,” alisema.
Credit: Majira