LAKI 3 YA MAHALI, WAZAZI WAZUIA NDOA KANISANI


Bwana harusi (kulia) akiwa na mpambe wake.
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
KATIKA  hali  isiyotarajiwa na wengi,  harusi iliyokuwa ifungwe jijini Mbeya Jumamosi iliyopita kati ya bwana harusi, Fadhili Mahenga (28) na bi. harusi Naomi Ngoje imeshindikana  baada ya mume mtarajiwa kushindwa kumalizia mahari ya shilingi laki tatu.
Waumini wakiwa kanisani kusubiri ibada ya ndoa.
Tukio hilo limetokea katika Kitongoji cha Makunguru, Mtaa wa Ilolo Jijini Mbeya na kusababisha sintofahamu  kwa familia ya mume mtarajiwa.
Mahenge ambaye ni mkazi wa Songea mkoani Ruvuma alishafuata hatua zote za kikanisa ili kuweza kumuoa Naomi katika Kanisa la Free Pentecoste Church Of Tanzania(FPCT) lakini alijikuta akishindwa kuamini kile kilichotokea baada ya mkewe kufungiwa chumbani na kuambiwa hamna ndoa mpaka amalizie mahari ya shilingi 300,000.
Bibi harusi akiwa chumbani baada ya kutokea sintofahamu hiyo.
Akizungumza na mwandishi wetu, nyumbani kwa familia ya bibi harusi,  mjomba wa bi harusi, Dickson Ngoje amesema wamegomea ndoa hiyo ili kuwataka waoaji watimize masharti waliyokubaliana awali ambayo hadi siku ya mwisho hawakuwa wameyatekeleza.
“Siku ya kwanza waoaji walifika nyumbani kwa mzee Ngoje na kujitambulisha, wakapangiwa utaratibu wa mahari kwa mujibu wa mila kuwa watatakiwa kutoa mablanketi mawili,  mashuka mawili, mkaja wa mama (Sh. 200,000), mbuzi wanne, majembe manne, ng’ombe majike wawili na ngo’mbe dume mmoja pamoja na fedha taslimu shilingi laki tatu.
...Baada ya mambo kuharibika.
“Lakini familia ya waoaji waliondoka na kuahidi kurudi siku nyingine kwa ajili kukamilisha vitu hivyo, kweli walikuja tena Septemba 11, mwaka huu wakiongozwa na mshenga mzee Katete wakiwa na mablanketi mawili,  mashuka mawili pamoja na Fedha shilingi 10,000 ambazo vilipokelewa na kuwaambia hawawezi kuzungumza chochote juu ya Ndoa hiyo mpaka wakamilishe vilivyobaki,” alisema mjomba huyo.
Mjomba huyo ameendelea kufafanua kwamba  baada ya wiki mbili waoji walirudi tena wakiwa na shilingi 200,000 ndipo walipoambiwa walipe kiingilio shilingi 100,000 ili waweze kupokelewa jambo ambalo walilitekeleza kisha wakalipa fedha walizokuwa nazo kama mkaja na kuomba wapewe kibali cha kuandikisha ndoa na taratibu za kumalizia vilivyobaki zikiendelea.
Ukumbini.

Mjomba huyo alisema kwamba  ndoa hiyo ilitangazwa  kanisani mara tatu kuanzia Desemba 8 hadi Desemba 22, mwaka huu.
Akiendelea kufafanua jambo hilo, mjomba huyo alisema kwamba  Desemba 23, mwaka huu  upande bi harusi walijikusanya na kupanga taratibu za sherehe  ya kumwaga binti yao (send off) ambayo ilifanyika Desemba 24, mwaka huu.
Kwa kuwa mahari ilikuwa  haijaisha, baadhi ya ndugu wa bi harusi wakaingiwa na wasiwasi kwamba familia ya bwana harusi haioneshi uaminifu wa kumalizia mahari iliyobaki ambayo ni shilingi 300,000, hivyo kumzuia binti yao kufunga ndoa.
Kwa upande wake, mchungaji aliyepangwa kufungisha ndoa hiyo ambaye pia ni Askofu wa Kanisa hilo, Kenan Mpalala alipoulizwa kuhusu hali hiyo alisema anawashangaa upande wa bi harusi mtarajiwa kutoa malalamiko kuhusu kutomaliziwa mahari jambo ambalo alidai kwamba halimhusu kwa kuwa lilitakiwa kumalizwa na pande mbili za wazazi wa wanandoa hao.
Naye bwana harusi, Mahenge akiwa kanisani kwa ajili ya kufunga ndoa alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema anachosubiri ni hatma ya wazazi wa bi harusi kama wanaweza kumwachia mkewe ili wanachodai aweze kuwamalizia  kwa awamu.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni timu ya usuluhishi ilikuwa ikiendelea na kazi yake ikiongozwa na askofu huyo


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...