TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ufafanuzi kuhusu Tume ya Katiba kutupiwa virago
Gazeti la Raia Mwema lililotoka leo, Jumanne, Aprili 2, 2014, limeandika habari zisizokuwa za kweli chini ya kichwa cha habari : “Warioba: Ikulu imetutupia virago”.
Habari hiyo inamkariri aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akidai kuwa Tume yake ilifukuzwa
kazi, kwamba haikupewa muda wa kuandaa na kuwasilisha nyaraka za
kukabidhi ofisi na madaraka na kwamba wajumbe wa Tume hiyo waliporwa
magari ambayo yamewekwa Ikulu.
Aidha, Gazeti la Mtanzania la leo pia, limeandika habari, zisizokuwa za kweli vile vile, chini ya kichwa cha habari: “Bilioni 6 kuipoza Tume ya Warioba”.
Habari hiyo inamkariri mjumbe mmoja wa Tume hiyo, ambaye Gazeti
halimtaji jina, akidai kuwa Tume hiyo inatarajiwa kupewa kiasi cha
Sh.bilioni sita ikiwa ni kiinua mgongo ambako kila mjumbe atapata kiasi
cha Sh. milioni mia mbili.
Habari zote mbili ni za uongo na Ikulu inapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
(a) Tume kufukuzwa kazi
Itakumbukwa kuwa moja ya mijadala mikali ya awali kuhusiana na mchakato
wa Katiba Mpya ulihusu lini Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize muda
wake; wengine wakitaka Tume imalize muda wake baada ya kukabidhi Ripoti
ya Tume na Rasimu ya Katiba, wengine wakitaka Tume imalize muda wake
baada ya Mwenyekiti wake Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu yake Bungeni na
hata wengine wakitaka wajumbe wa Tume wawe sehemu ya Bunge Maalum la
Katiba.
Hatimaye, ilikubaliwa kuwa Shughuli za Tume zingefikia ukomo wake baada
ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la
Katiba kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba.
Kifungu hicho kinasema kuwa baada ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba
kwenye Bunge Maalum chini ya Kifungu cha 20(3) (cha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba) Rais, kwa Amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali,
atavunja Tume.
Mheshimiwa Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum la
Katiba Jumanne ya Machi 18, mwaka huu, 2014 na siku iliyofuata Jumatano,
Machi 19, 2014 na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais
alitia saini tangazo la Serikali la Kuvunja Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Tangazo hilo lilichapishwa katika toleo lililofuata la Gazeti la
Serikali la Ijumaa, Machi 21, 2014. Gazeti la Serikali huchapishwa kila
Ijumaa ya kila wiki.
Hivyo, tokea mwanzo wa mchakato mzima wa Katiba Mpya na utendaji kazi wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapakupata kuwepo, hata wakati mmoja,
shaka kuhusu siku ya Tume hiyo kumaliza kazi zake. Mwenyekiti wa Tume,
wajumbe wote wa Tume, Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua
fika siku ya mwisho ya Tume kukamilisha shughuli zake. Kwa mtu kujitia
ameisahau siku hiyo leo ni kiwango cha juu sana cha unafiki.
Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka wala mamlaka yoyote kubadilisha
tarehe hiyo. Hivyo, madai ya Ikulu kuitupia virago Tume ya Mabadiliko ya
Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la kutunga tu.
(b) Muda wa kuandaa na kukabidhi nyaraka na ofisi
Hili nalo ni jambo la kutunga na kuzusha tu. Mheshimiwa Jaji Warioba
alikabidhi rasmi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa
Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Jumatatu ya Desemba 30,
2014, mbele ya wananchi viwanja vya Ukumbi wa Karimjee, Dar Es Salaam.
Hivyo, tokea siku hiyo, Tume haikuwa tena na kazi ya kuandaa Ripoti ama
Rasimu kwa sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha na wala isingeweza
kuibadili tena Rasimu ya Katiba. Kwa maana hiyo, tokea Desemba 30, mwaka
jana, kupitia miezi ya Januari, Februari mpaka Machi 18, mwaka huu,
Sekretariati ilikuwa na muda wa siku 77, zaidi ya miezi unusu, kufanya
maandalizi ya kukabidhi nyaraka na ofisi kwa sababu ilijua kazi yake
ilikuwa inamalizika siku ambayo Mwenyekiti wa Tume hiyo angewasilisha
Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum la Katiba.
Sasa katika muda wote huo, Sekretarieti ya Tume ilikuwa inafanya nini
badala ya kuandaa ripoti ya makabidhiano na wakati maofisa wake walikuwa
wanaendelea kulipwa mshahara na Serikali? Kwa nini walalamike hadharani
leo kwa jambo ambalo lilikuwa ni la wajibu wao na wakashindwa kulifanya
kwa wakati?
(c) Wajumbe wa Tume kutakiwa kurudisha magari Ikulu
Ni kweli kuwa wajumbe wa Tume walitakiwa kurudisha Ikulu magari ambayo
walikuwa wanatumia kikazi kwa sababu kazi ya Tume ilikuwa imemalizika.
Pili, Tume ilijua tokea mwanzo kuwa baada ya kumaliza kazi yao, magari
ambayo walikuwa wanatumia wajumbe na maofisa wa Tume hiyo yalikuwa
yanatakiwa kupelekwa Dodoma kwa matumizi ya shughuli za Bunge Maalum la
Katiba ambalo linakabiliwa na shida kubwa ya usafiri.
Serikali ilichukua uamuzi kuwa magari hayo yapelekwe Dodoma kwa sababu
lisingekuwa jambo la busara kwa Serikali kutumia fedha za umma kununua
magari mengine mapya wakati yale ya Tume bado yanafaa kufanya kazi na
wala hakuna bajeti ya kufanya manunuzi ya magari mapya.
Hivyo, ni kweli magari hayo yako Ikulu, Dar es Salaam, yakisubiri
kukamilika kwa taratibu za kuyapeleka Bunge Maalum la Katiba mjini
Dodoma.
(d) Wajumbe wa Tume kulipwa kiinua mgongo cha Sh.milioni 200 kila mjumbe
Hakuna shaka kuwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wamefanya kazi
nzuri sana na wanastahili pongezi nyingi za wananchi. Lakini kama
wanadhani kuwa Serikali ina uwezo wa kumlipa kila mjumbe kiinua mgongo
cha Sh. milioni 200 basi wanajidanganya. Wala wananchi wa Tanzania
hawawezi kuelewa maana kabisa ya malipo hayo makubwa kupindukia.
Alichokizungumza Rais Kikwete tokea mwanzo wa mchakato ni kwamba
atafikiria kuwalipa wajumbe wa Tume aina fulani ya kifuta jasho ambacho
kiwango chake atakiamua yeye na kwa wakati mwafaka na kulingana na
raslimali za Serikali. Mpaka sasa hajafanya uamuzi juu ya jambo hili.
(e) Posho ya Sh.500,000 kutwa kwa kila mjumbe wa Tume
Ikulu pia inapenda kutoa ufafanuzi wa habari zinazosambazwa na baadhi ya
vyombo vya habari kuwa wajumbe wa Tume hiyo walikuwa wanalipwa Sh.
500,000 (Laki tano) kama posho ya vikao kwa siku. Hili nalo siyo la
kweli.
Ukweli ni kwamba wajumbe wa Tume walikuwa wanalipwa Sh. 200,000 kama
posho ya vikao kwa siku. Maofisa waandamizi wa Tume hiyo walikuwa pia
wanalipwa posho ya Sh. 200,000 (Laki mbili) kwa siku, maofisa wa kati
walikuwa wanalipwa Sh. 150,000 kutwa na maofisa wa ngazi za chini
walikuwa wanalipwa Sh. 100,000 kwa siku kulingana na taratibu za
Serikali. Anayetangaza vinginevyo anajaribu tu kuwapotosha wananchi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
02 Aprili, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)