WAZIRI MWAKYEMBE AIBUKA BANDARINI, AITUPIA LAWAMA TRA

 
Na Ibrahim Yamola, MwananchiDar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameitupia lawama Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kwa kile alichokieleza kulala kwao siku za mapumuziko na sikukuu kunarudisha nyuma ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati wa ziara ya kikazi bandarini hapo akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Omari Issa.
Mwakyembe alisema watendaji na viongozi wa bandari, wamekuwa wakifanya kazi saa 24 ili kuhakikisha meli zinashusha mizigo haraka na wahusika wanachukua mizigo hiyo pasipo vikwazo.
“Bandari wanafanya kazi saa 24 kwa siku saba za wiki bila kupumzika, lakini wenzetu wa TRA wao sikukuu na siku za mwisho wa juma wanalala hali hii inaturudisha nyuma kimapato,” alisema Dk Mwakyembe.
Aliongeza: “Nchi bado ipo nyuma, tunahitajika kuchapa kazi usiku na mchana kuhakikisha tunasonga mbele na hii itafanikiwa ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo.”
Alisema kama TRA wataanza kufanya kazi kila siku, hakuna shaka kwamba taasisi za fedha (benki) nazo zitaiga hatua hiyo.
“Huwezi kusema kufanya kazi kila siku watahitaji kuongezewa fedha, hapana kwani wanalipwa fedha nyingi. Nitaendelea kufanya mawasiliano nao kuona ni jinsi gani suala hili tunaweza kulimaliza.”
Aidha, amewataka wamiliki wa Bandari Nchi Kavu (ICDs), kufanya kazi ya kutoa mizigo ya wateja wao kila siku ili kuepusha usumbufu usio wa ulazima.
“Unakuta mtu anahitaji kutoa mizigo yake lakini wahusika siku za mapumziko hawafanyi kazi. Kwa nini wasifanye kazi kila siku kama bandari,” alihoji Mwakyembe.
Naye Mtendaji Mkuu wa BRN, Omari Issa alisema ameamua kufanya ziara hiyo kujionea changamoto wanazokutana nazo ili kuona ni jinsi gani wataweza kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari, Awadhi Massawe alisema changamoto wanazokabiliana nazo ni ufinyu wa maeneo ya kuhudumia meli na kuhifadhi shehena za mizigo.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...