YEAH, DIAMOND ANA MATATIZO


NASIBU Abdul ndilo jina lake, lakini mashabiki wake na wale wa muziki wa kizazi kipya kwa jumla, wanamtambua kama Diamond Platnumz, nyota wa Bongo Fleva ambaye anafanya vizuri zaidi kwa sasa, pengine kuliko mwingine ye yote.
Ni kijana mdogo bado kimuziki, kwani tokea ameanza kukamata chati, hana hata miaka minne. Niweke wazi kuwa sijawahi kuzungumza na msanii huyu, hanifahamu, ingawa mimi ninamfahamu kupitia kazi zake.
Katika kipindi hicho kifupi, amefanya mambo mengi, mazuri na kiasi mabaya. Mazuri kwa sababu amemudu kukaa kileleni kwa muda wote huo, aking’ara karibu kwa kila kibao anachokitoa. Binafsi nilianza kumtambua baada ya kutoka na wimbo wake wa Mbagala.
Tokea wakati huo hajawahi kuwaangusha mashabiki wake, kwani siyo tu amekuwa akiimba vizuri, bali hata yeye mwenyewe awapo jukwaani, anaonyesha kujituma. Huenda anatambua kuwa muziki ni kazi yake, hivyo lazima awajibike, tofauti na baadhi ya wasanii wanaoleta pozi jukwaani!
Wafuatiliaji zaidi wa Bongo Fleva wanafahamu kazi zake, lakini ninazozifahamu mimi si nyingi kama Kamwambie, Nitarejea, Mawazo, Nataka kulewa na sasa Number One.
Na huenda anaweza kuwa msanii wa kwanza kuwa na vibao vingi vilivyo-hit, licha ya kwamba yeye mwenyewe ana muda mchache tu katika game. Hutokea, msanii akafanya vizuri kwa kibao chake kimoja au viwili, baada ya hapo anakuwa wa kawaida tu.
Hii ndiyo sababu inayomfanya kuwa mmoja kati ya wasanii wachache wanaolipwa fedha nyingi zaidi kwa shoo moja. Ni mchapakazi, hana nyodo kazini!
Lakini katikati ya sifa hizi, kijana huyu ana baadhi ya mambo ya kushangaza ambayo yanamuondolea hadhi anayostahili. Ningependa kuzungumzia masuala ya kikazi zaidi kwa sababu kwa kadiri nijuavyo, kila mtu ana mapungufu yake katika maisha binafsi.
Hili tatizo la kupigiwa kelele za wizi wa kazi za wenzake!
Ni jambo la kusikitisha sana kuona supastaa wa aina yake, akipigiwa kelele hizi kila kukicha. Alianza H. Baba, aliyelalamika kuibiwa mashairi yake yaliyotengeneza wimbo wa Nataka kulewa. Utetezi wake haukushawishi, kwamba eti haikuwa kweli isipokuwa aliyetoa tuhuma hizo alikuwa anataka kujipatia umaarufu kwa kutumia jina lake.
Sijui, lakini sidhani kama kuna shabiki wa kweli wa muziki huu anaweza, siyo tu kukubali, bali hata kufikiria kwamba H Baba anatafuta umaarufu kupitia kwa Diamond.
Kwamba alikuwa na tabia hii, ilidhihirika pia wasanii wengine nao walipojitokeza na kutoa madai kama hayo, wengine wakisema wameibiwa mashairi, wengine beat. Ninajua si kila mwimbaji mzuri basi ni mtungaji mzuri. Kuna watu kazi yao ni kutunga tu mashairi ya nyimbo na wanalipwa kwa ajili hiyo.
Huenda Diamond hajui kutunga. Kama ndivyo, hili siyo kosa wala dhambi. Kuna wanamuziki wengi tu wakubwa duniani hawajui kutunga, wana watu wao wa kuwaandikia nyimbo, wao kazi yao ni kuimba tu.
Lakini tatizo zaidi lilikuja baada ya kutakiwa kujibu shutuma hizi. Huenda ni utoto, kulewa sifa au uelewa mdogo. Kwamba ili kuondoa kelele hizi, basi kuanzia sasa hatakubali kushirikishwa na wasanii wenzake, hasa underground!
Nakumbuka kauli kama hii iliwahi kutolewa na msanii mwingine aliyeibuka miaka flani ya katikati ya 2000 ambaye sasa ni supastaa mkubwa. Nakumbuka pia niliwahi kuandika kuelezea masikitiko yangu. Dawa ya kuondoa kelele za wizi siyo kuacha kushiriki au kushirikisha, bali ni kuacha tabia hiyo.
Hakuna mwanamuziki anayeweza kufanya kazi peke yake bila kushirikisha au kushirikishwa. Pamoja na utajiri wao, uwezo wao mkubwa wa kazi, P. Diddy, Jay Z na hata marehemu Michael Jackson, walishirikishwa au kushirikisha wenzao katika kazi.
Dawa ya kuacha udokozi si kuhama nyumba kuepuka kelele, bali kuacha tabia hii ambayo mwishowe inaweza kuleta madhara. Kuna wakati anaweza kuiba mashairi ya mtu mwenye msongo wa mawazo ikawa balaa!
Nasikia wanasema kijana ana fedha nyingi, sijui. Lakini kama kweli anazo na bahati mbaya hajui kutunga, atangaze bingo, watungaji wapo wengi tu Bongo na kama hatajali, hata mimi naweza kumpatia watu wa namna hiyo!


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...