ATHARI ZA MAUMIVU YA MUDA MREFU YA KIFUA (HEART ATTACK)

 
TUMEONA kwa undani dalili za maumivu ya kifua katika toleo lililopita, ingawa  maumivu haya husababishwa na magonjwa mbalimbali kama pumu na nimonia, lakini tumelenga kuzungumzia  matatizo ya moyo ambayo kwa kiasi kikubwa ni matatizo yanayosahaulika na mtu akihisi ni tatizo jingine kumbe mwisho wa siku hali inakuwa mbaya.
‘Heart Attack’ ni hali  ya moyo kushikwa, kuzuiliwa kufanya kazi na huambatana na maumivu makali sana ya kifua tofauti na yale ya ‘Angina Pectoris’. Mgonjwa anaweza kuanguka na kuzimia au kupoteza maisha ghafla.
Matatizo haya au athari hii ni muendelezo wa tatizo la maumivu ya kifua yanayoambatana na  kuchoka na kuumwa kuumwa kama tulivyozungumzia katika makala iliyopita.

Chanzo cha tatizo
Moyo hushikwa au kuzuiliwa kufanya kazi ya kusukuma damu mwilini husababishwa na misuli ya moyo kunyauka au kufa kutokana na kukosa mzunguko wa damu ambapo kitaalamu huitwa ‘Myocardial infarction’.

Misuli ya moyo inakufa au inashindwa kufanya kazi endapo mishipa ya damu inayoizunguka itaziba ‘Obstruction in a coronary artery.’ Hii inatokana na damu kuwa nzito sana au kuganda  ndani ya mishipa au kuwepo na kiwango kikubwa cha mafuta ndani ya mishipa ya damu. Hivyo damu inashindwa kusambaa katika misuli ya moyo.
Dalili za tatizo
Utajuaje kwamba sasa unaanza kupata ‘Attack’ au moyo unaanza  kubanwa?
Utahisi dalili kama zile za ‘Angina Pectoris’ ambapo kifua  kinauma na  maumivu yanasambaa hadi mgongoni na mabegani, unapata uchovu na unaanza kupiga mihayo, jasho linakutoka na hali inakuwa mbaya zaidi kifuani na siku zote.
Hali hiyo huendelea kwa muda na unahisi hewa haitoshi, unatokwa na jasho zito huku ukihisi baridi, moyo unaenda mbio na kubanwa na pumzi na unahitaji ulale.

Mgonjwa ataanza kukohoa na kupata kwikwi na kuhisi kiu kali ya maji, shinikizo la damu litashuka na atahisi haja ndogo akipata inatoka kidogo sana. Endapo mgonjwa atapata msaada wa kumweka vizuri kumlaza chali na kunyanyua kifua na kichwa kwa kumwekea mito, anaweza kupata nafuu na ukamuwahisha hospitali.
Endapo hali kama hii na utaamua kumkimbiza mara moja hospitali bila ya kumpatia msaada  wa kupumua vizuri ili kuwezesha msukumo wa damu uende vizuri, basi mgonjwa anaweza kufariki akiwa njiani kuelekea hospitali.
Ukubwa wa tatizo
Tatizo huwapata zaidi watu walio katika umri wa kati miaka kuanzia 35 hadi 45 na umri wa zaidi ya miaka 45 tatizo pia hutokea na hali huwa mbaya zaidi.

Tatizo huanza taratibu katika umri chini ya miaka 35 hasa kwa watu wanene hali ndiyo huwa mbaya zaidi.
Wanawake na wanaume wote huathirika.
Watu wenye tatizo la juu la shinikizo la damu kwa muda mrefu, wagonjwa wa kisukari, wavuta sigara na walevi pia huathirika kwa kiasi kikubwa.

Uchunguzi wa tatizo
Hufanyika katika hospitali za wilaya na mikoa, wahi hospitali unapohisi kuchoka hasa baada ya tendo la ndoa.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...