BODI YA MIKOPO YAKUSANYA BILIONI 20/-

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru.
Bodi  ya Mikopo nchini, imeboresha mfumo wake wa makusanyo ya malipo ya mikopo inayotolewa kwa wanafunzi na kufanikiwa kukusanya Sh. bilioni 20 mwaka jana.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akifungua mkutano wa siku tatu wa Umoja wa Taasisi zinazokopesha wanafunzi wa vyuo vikuu na elimu ya juu Barani Afrika unaofanyika jijini hapa.
Alisema hali ya urejeshwaji wa mikopo ni nzuri kwa sasa kwani asilimia 61 ya fedha zinazokopeshwa zinarejeshwa na kusaidia kukopesha wanafunzi wengine.Dk. Kawambwa alisema kuwa hali imekuwa tofauti na siku za nyuma.
Aidha, alisema mwaka wa fedha mwaka huu, serikali imetenga Sh. bilioni 326 kwa ajili ya kukopesha wanafunzi. “Lakini tunatarajia hata mwaka huu mwishoni tutakuwa tumekusanya Sh. bilioni 20 na hii itaendelea kupanda kwa sababu bado kuna watu hawajarejesha," alisisitiza.
Kuhusu kuwashtaki wanafunzi ambao walikopeshwa na kutorejesha pindi wanapopata kazi, alisema hawapendi sana kupelekana mahakamani kwa sababu inapoteza muda wa kufuatilia kesi, japo wapo baadhi wamepelekwa mahakamani.
Aliwaomba wanafunzi na wafanyakazi waliosoma kwa mikopo hiyo, wakumbuke kurejesha ili kuwezesha  wenzao kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu.
Naye Mkurugenzi wa Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini, George Nyatega, alisema kwa sasa Bodi hiyo inatoa mikopo asilimia 48 ya wanafunzi wote wanaosoma elimu ya juu na wanaobakia wanajisomesha wenyewe.
Alisema wanatamani kukopesha watu wengi zaidi lakini fedha walizonazo ni hazitoshelezi na ndiyo maana wanasisitiza urejeshwaji wa fedha hizo kwa waliomaliza.
“Tunajua malalamiko yapo mengi, lakini lazima yawapo kwa sababu wapo watu hawakidhi vigezo vyetu na fedha kuwa kidogo," alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Umoja  wa Taasisi zinazokopesha wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu (Ahefa), Charles Ringera, alisema umoja huo unalenga nchi zote za Afrika zijiunge ili wawafuatilie watu waliokopeshwa kupitia bodi za kila nchi warejeshe fedha hizo kwa nchi yoyote alipo kwa wakati huo.

                                                                  CHANZO: NIPASHE


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...