Watuhumiwa wawili wa kesi ya mauaji
dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John
Mwankenja, Kelvin Myovela(kushoto), aliyehukumiwa kifungo cha miaka saba jela
na David Mwasipasa(Kulia) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana
na hatia katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya.
Mhukumiwa namba moja wa kesi ya
mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Hakimu
Mwakalinga(kushoto) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa na mwenyeshati la Bluu ni
Obote Mwanyingili amehukumiwa miaka saba jela kwa kumhifadhi mtuhumiwa.(Picha na Ezekiel Kamanga, Mbeya)
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
WATUHUMIWA wawili kati ya wanne
wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, wamehukumiwa
kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama kuu kanda ya
Mbeya.Hukumu hiyo ilitolewa jana katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya iliyokuwa ikiendesha vikao vyake katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe chini ya Jaji Samweli Karua, baada ya kuahirishwa kutolewa kwa hukumu hiyo kwa zaidi ya mara tatu na kuzua hali ya sintofahamu kwa ndugu wa washtakiwa na wafuatiliaji wa kesi hiyo.
Awali kabla ya kusoma kwa
hukumu hiyo Mwendesha mashtaka wa Serikali., Archiles Mulisa, aliwataja
watuhumiwa wote wanne kuwa ni Hakimu
Mwakalinga, Daudi Mwasipasa, Obote Mwanyingili na Kelvin Myovela wanaokabiliwa
na tuhuma za kumuua kwa maksudi aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Rungwe John Mwankenja.
Alisema watuhumiwa hao wenye kesi
namba 131/2012 walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika kijiji cha Mpandapanda,
Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Mulisa aliyekuwa akisaidiwa na
Wakili wa Serikali Lugano Mwakilasa kwa upande wa mashtaka huku Watuhumiwa wakitetewa na Mawakili wawili ambao
ni Victor Mkumbe na Simon Mwakolo.
Mulisa alidai mahakamani hapo kuwa
kesi inayowakabili watuhumiwa hao walilitenda Mei 19,2011 kwa kumuua kwa
maksudi John Mwankenja kinyume na kifungu cha 196 sura ya 16 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Aliongeza kuwa pande hizo mbili pia
hazibishaniwi kuhusu ripoti za kitaalamu na dhamira za mauaji hayo bali
kinachobishaniwa ni uhusika wa watuhumiwa hao dhidi ya mauaji hayo.
Alisema katika kutetea hoja zao
upande wa mashtaka ulileta mashahidi 11 ambao wote kwa pamoja wakiongozwa na shahidi namba moja
waliwatuhumu washtakiwa kuhusika na tukio hilo.
Shahidi huyo namba moja Weston
Jacob(17) mkazi wa Kiwira Mwanafunzi kidato cha Tatu katika shule ya Sekondari
Kipoke ambaye pia ni Mjomba wa marehemu ambaye aliiambia mahakama kuwa siku ya
tukio akiwa nyumbani akijisomea majira ya 2: 30 usiku ambapo marehemu alifika
nyumbani na kupiga honi ya gari akitaka afunguliwe mlango.
Kutokana na ushahidi huo alisema
Mshtakiwa namba moja na namba mbili ambao ni Hakimu Mwakalinga na Daudi
Mwasipasa wanatiwa hatiani kuhusika moja kwa moja na mauaji kutokana na ukiri
wao kwa mlinzi wa amani, Mchukua maelezo na vipimo vya vinasaba.
Alisema Mshtakiwa namba tatu Obote
Mwanyingili yeye anatiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba
moja baada ya kutoka kufanya mauaji hivyo yeye hausiki moja kwa moja na kosa
hilo.
Jaji karua alisema kwa upande wa
mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela anatiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha
iliyotumika nkatika mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja.
Aliongeza kuwa kutokana na kifungu
cha sheria cha mwenendo wa makosa ya jinai kifungu namba 300 na 217 washtakiwa
namba tatu na namba nne wanatiwa hatiani na mahakama.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa, aliiambia
mahakama hiyo kwamba itoe adhabu kali kutokana na kitendo alichofanyiwa
marehemu na iwe fundisho kwa watu wengine.
Kwa upande wa utetezi ambao siku ya hukumu uliwakilishwa na
Wakili Merick Luvinga alisema mahakama iwanee huruma washtakiwa kwa kuwa wote
umri wao ni mdogo wanaweza kujifunza na kurudi kuungana na jamii pia ni kosa
lao la kwanza hivyo wasipewe adhabu kali.
Kutokana na utetezi huo, Jaji Karua alisema kutokana na
ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuthibitisha kuhusika pasipo shaka kwa
washtakiwa namba moja na namba mbili hivyo adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.
Aliongeza kuwa Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili
anayehusika kumhifadhi mtuhumiwa wa kwanza ataenda jela miaka saba kwa kosa
hilo sambamba na mshtakiwa namba nne
Kelvin Myovela aliyehifadhi silaha iliyotumika kwenye mauaji.