ZITAMBUE NDEGE NNE ZILIZOWAHI KUPOTEA TANZANIA



Wananchi wakiangalia ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa katika Uwanja wa Ndege wa Arusha, baada ya kushuka kwenye uwanja huo mdogo kimakosa hivi karibuni. Picha ya Maktaba
Wakati tukio la kupotea kwa ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia, MH370, linaendelea kuitikisa dunia, imebainika kuwa Tanzania si jambo jipya kutokana na kuwapo kwa kumbukumbu ya matukio manne tofauti kama hayo katika miongo minane iliyopita.
Ndege hiyo ya Malaysia ilipotea wiki mbili zilizopita ikiwa na abiria 227 na wafanyakazi 12 huku juhudi za kuitafuta zinazofanywa na nchi 26 zenye uwezo mkubwa wa kiuchunguzi zikiwa hazijazaa matunda.
Kwa matukio ya Tanzania, Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihura amesema katika mahojiano maalumu na mwandishi wetu kuwa Tanzania imewahi kuingia katika kumbukumbu za ndege ndogo kupotea na  baadhi hazikuonekana kabisa na nyingine zilionekana baada ya miaka kadhaa kupita. Ndege ya kwanza kupotea ilikuwa mwaka 1937 iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda Madagascar. Ilikuwa na abiria wanane na haijaonekana hadi leo.
Mbali na tukio hilo ambalo limedumu kwa miaka 77 sasa, Nyamwihura alisema tukio la pili ni la mwaka 2003 wakati ndege iliyokuwa ikitoka Tanzania kwenda Zambia ilipopotea ikiwa na raia wawili wa Afrika Kusini, nayo pia haijaonekana hadi sasa.
Mkaguzi huyo alisema katika matukio mengine mawili, ndege zilizopotea zilionekana baadaye. Mwaka 1997, ndege ndogo iliyokuwa na abiria mmoja ilipotea katika bonde kwenye kilele cha Kibo, Mlima Kilimanjaro baada ya kutumbukia kwenye korongo na kuganda kwenye barafu bila kuonekana hadi baada ya miaka sita. Hata ilipoonekana haikuwezekana kutolewa.
“Ndege ile ilikuwa ikitoka Nairobi kwenda Zanzibar ikiwa na rubani wa Kitanzania peke yake,” alisema Nyamwihura.
Ndege nyingine iliyoingia katika orodha hiyo ni ile iliyoanguka katika Ziwa Victoria mwaka 1976 ikiwa na abiria 12 ambayo ilionekana miaka miwili baadaye.
Kwa nini ndege zinapotea?
Swali hili linajibiwa na Nyamwihura akisema sababu kubwa ya matukio hayo ni mabadiliko ya hali ya hewa na kuharibika kwa miundombinu, mambo ambayo husababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani.
“Matukio mengi kama haya ni kuwa ndege hugonga milima na kuanguka. Zikianguka sehemu za milima ni vigumu kupatikana kwa sababu wakati mwingine huganda katika barafu au kuzama kwenye makorongo,” alisema.
Alisema hata ndege zinazoanguka kwenye maji, pia ni vigumu kuonekana kutokana na kina kirefu au barafu.
Mtaalamu huyo alisema kuna baadhi ya ndege ambazo hupotea kutokana na rubani kukata mawasiliano kwa makusudi kwa sababu ama za kigaidi au magendo.
Alitoa mfano wa tukio la mwaka 1945, wakati ndege iliyokuwa ikitoka Malawi kwenda Nairobi, ilipopoteza mawasiliano ikiwa katika anga la Tanzania. Baadaye ilibainika kuwa rubani alifanya hivyo kwa makusudi ili ashushe bidhaa za magendo alizokuwa amepakia.
Sheria za anga za Tanzania zinakataza rubani kukata mawasiliano kwa makusudi na adhabu yake ni kufungiwa kabisa shughuli za urubani.
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, Moses Malaki alisema kwa kawaida ndege zinapokuwa angani hufuata ‘barabara’ ambazo zipo kama miduara inayoonyesha mpaka wa eneo moja kuingia jingine. “Katika hali ya kawaida, rubani huwasiliana kwa njia ya nukushi (fax) ili vituo vya eneo husika ambalo ndege hupita vipate taarifa,” alisema Malaki.
“Endapo rubani atashindwa kuunganisha mawasiliano kutoka eneo moja na jingine na ikitokea kuna miundombinu mibovu katika eneo hilo, basi ndege inaweza isionekane na kupotea,” alisema.
Malaki alisema asilimia 95 ya ndege huanguka au kupotea kwa sababu ya makosa ya kibinadamu na wala si makosa ya kimitambo akisisitiza kuwa ndege ndiyo usafiri ulio salama zaidi duniani.
Chanzo ajali za ndege
Rubani Mtanzania anayeishi Marekani, Brian Meena alisema katika mahojiano kuwa chanzo cha ajali nyingi za ndege nchini ni makosa ya kibinadamu na wala si mitambo.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa wengi wanaopata ajali hizo ni marubani wazoefu na wala si wanafunzi.
 “Kwa mfano, unapokuwa na saa nyingi za kuendesha ndege lazima uchoke, watu wengi wanaoangusha ndege ni wale wanaotumia muda mrefu hewani,” alisema. Meena alitaja sababu nyingine kuwa ni miundombinu chakavu ya viwanja vya ndege na mara chache ndege zenyewe.
“Inawezekana kabisa kuwa mamlaka ya ndege inafanya kazi kwa mazoea au kienyeji. Wanatumia njia za kizamani za usimamizi wa usafiri huu na hawaendi na wakati kwa kununua vifaa vya kisasa,” alisema.
Alisema usafiri wa ndege ni salama kwa asilimia 99 kutokana na mafunzo ya kina marubani wanayopewa.
“Ndege ni kama mtoto, unamlea, unampa anachotaka na ukifanya hivyo ajali labda itokee kwa miujiza,” alisema.
 MWANANCHI


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...