MBUNGE AHOJI SABABU WANANCHI KUKATWA KODI ZA SIMU KINYEMELA

 
Spika wa Bunge,Anne Makinda.
Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), ameitaka serikali ieleze kwa nini wananchi watozwe kodi na kampuni za simu bila wenyewe kujua.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Haji aliomba mwongozo wa Spika kupata maelezo kufuatia kauli ya Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, kuwa zipo kampuni za simu za mikononi ambazo huwatoza wananchi kodi nyingine bila wenyewe kufahamu.
Katika swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Ritha Kabati (CCM), kuhusu kodi zinazotozwa na kampuni ya simu, Naibu Waziri Mbene alisema zipo nyingi na hata nyingine zinatozwa bila wananchi kujua.
Hata hivyo, Spika Anne Makinda, alimtaka mbunge huyo kama ana shaka au hajaridhika na majibu ya waziri, amwandikie barua Spika kupata maelezo ya ziada.
Katika swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Tauda Gallos (CCM), alitaka kujua ni kodi gani mpya zimependekezwa kwa mwaka huu wa fedha na kiasi gani cha mapato ya ziada kimetolewa kukusanywa.
Akijibu, Naibu Waziri alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/14, serikali imeanzisha kodi ya Sh. 50 kwa lita kwenye mafuta ya petroli na dizeli kugharimia kusambaza umeme vijijini na kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia tano kwenye huduma za ushauri.
 
CHANZO: NIPASHE


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...