Msafara wa JK nusura upate ajali ya kugonga treni

Katika hali isiyo ya kawaida, msafara wa Rais Jakaya Kikwete juzi ulinusurika kupata ajari eneo la Gold Star, eneo la Gerezani, Kariakoo, Dar es Salaam.
Msafara huo ulitaka kugonga kichwa cha treni inayotumia reli ya kati wakati msafara wa Rais Kikwete ukitokea Ikulu, kupitia Barabara ya Mnazi Mmoja, kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Julius Nyerere.
Rais Kikwete alikuwa safarini kwenda nchini Marekani ambapo wakati msafara ukiwa eneo la Gold Star, pikipiki moja iliwahi kuvuka reli na treni ilikaribia kuvuka barabara.
Askari wa Usalama Barabara alijaribu kukisimamisha kichwa cha treni bila mafanikio wakati mfanyakazi wa reli katika eneo akitaka kufunga geti (kizuizi), ili msafara huo usimame.
 Jitihada za mfanyakazi wa reli hazikuzaa matunda baada ya askari wa usalama barabarani, kumkataza hivyo msafara huo ulifika karibu na kutaka kukigonga kichwa hicho.
Baada ya kutokea mkanganyiko huo kati ya trafiki na mfanyakazi wa reli, ghafla alitokea askari mwingine wa usalama barabarani na kuusimamisha msafara wa Rais Kikwete ili kichwa hicho kipite.
Hata hivyo, gari ya kwanza ya msafara ilisimama umbali wa mita tatu kutoka eneo ambalo kichwa hicho kilikuwa kikipita ambapo watu waliokuwepo eneo hilo walibaki kuduwaa na kutoamini kilichotokea machoni mwao.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema hali hiyo imechangiwa na ukosefu wa mawasiliano kati ya trafiki na mfanyakazi wa Kampuni ya Reli nchini (TRL).
"Isingekuwa trafiki kufanya uamuzi wa kuusimamisha msafara wa Rais Kikwete, ungekigonga kichwa hicho," walisema.
Majira lilizungumza na mfanyakazi wa reli, Bw. Kassimu Rai ambaye alisema askari wa usalama barabarani wamekuwa wakifanya makosa mengi katika misafara ya viongozi.
"Trafiki alifanya makosa kulisimamisha treni kwa mikono bila ya kuwasiliana na mimi...sheria za usafiri wa treni hawazijui ndiyo maana halikusimama," alisema Bw. Rai.
Alisema kama walijua kuna msafara, walitakiwa kumpa taarifa ili aweze kufanya mawasiliano mapema

Chanzo;Majira


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...