WAZIRI KAGASHEKI AJIUZURU; DAVID MATHAYO, NCHIMBI NA NAHODHA WATIMULIWA NA RAIS KIKWETE!

Mawaziri walioenguliwa 
MASHAMBULIZI ya wabunge dhidi ya mawaziri wanne kushindwa kusimamia wizara zao, yamemfanya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao kuanzia jana.
Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mathayo David Mathayo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Awali kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hajalieleza Bunge, uamuzi huo wa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Kagasheki alitangaza kujiuzulu wadhifa wake baada ya kuguswa na ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyokuwa ikichunguza madhila yaliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Balozi Kagasheki, ameamua kujiuzulu wadhifa wake baada ya kutuhumiwa kushindwa kusimamia kikamilifu Operesheni Tokomeza Ujangili iliyokuwa ikifanywa na wizara yake.
Alisema amesikiliza kwa makini sana ripoti ya kamati hiyo na kuamua kuachia wadhifa huo kutokana na madhila yaliyowapata watu, mifugo na mali.
“Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliponiteua alifanya hivyo kwa furaha yake na kuamini nitafanya kazi yake vizuri, yametokea yaliyotokea na yamesemwa mengi… mimi ni mtu mzima nimesoma hisia zenu.
“Nimeamua kujiuzulu wadhifa wangu na nitafuata taratibu zote zinazotakiwa… nitaitaarifu mamlaka ya juu uamuzi wangu,” alisema.
Mara baada ya Kagasheki kutoa taarifa yake hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo, alipopata fursa ya kuzungumza, alisema anaona anaonewa kuhusishwa na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na askari waliokuwa kwenye operesheni hiyo.
Aliongeza kuwa kutajwa kwake katika ripoti hiyo kunaonyesha watu walikuwa wana dhamira mbaya dhidi yake.
“Jana usiku nilisoma sana Biblia ambayo ni Zaburi ya 72… nilisali sana jana usiku kwakuwa niliona dalili za kuonewa, nawaambia matatizo mengi yaliyozunguzwa hayakuwa chini ya wizara yangu.
“Kuna wabunge wamesema wazi wazi hapa kuwa ninaonewa kuingizwa katika mkumbo wa mawaziri wanaotakiwa wawajibike, naapa mbele ya mwenyezi Mungu Subhana wa taala atawalipa wale walioona ninaonewa kwani nilijua hili,” alisema.
Mara baada ya Mathayo kuzungumza, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipewa fursa ya kuzungumza ambapo alisema amezungumza na Rais Kikwete ambaye yupo nchini Marekani juu ya jambo hilo na aliungana na wabunge waliokuwa wakitaka mawaziri hao wawajibike.
Alibainisha kuwa Rais Kikwete pia alitaka kuundwa kwa tume ya kuchunguza madhila yote yaliyotajwa kwenye ripoti ya kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata hilo.
“Nilipomueleza mambo hayo akasema ametengua uteuzi wake kwa mawaziri wote wanne, atakuja kuangalia hapo baadae kwa picha iliyojitokeza. Rais kaona uzito wa tukio hilo, hivyo kaamua kutengua uteuzi wao.
“Tumekubaliana na Rais Kikwete ambaye sasa yupo safarini, akirudi tutakuja kumalizia mambo yaliyobakia… mawaziri hawa wamejiuzulu si kwamba walikuwapo kwenye ameneo ya tukio au walishiriki bali vyombo vilivyofanya hivyo vipo chini yao,” alisema.
Pinda alisema pia alizungumza na mawaziri hao juu ya tuhuma zilizoelekezwa kwao na wabunge pamoja na kamati iliyoundwa na kuchunguza sakata hilo.
“Nilizungumza nao kwa jambo hilo, niliwaambia wabunge wamesema sana, niliwambia kwakuwa wao ni watu wazima wapime mambo hayo, waheshimiwa hawa wote wamekubali kujiuzulu, wamekubali kujiuzulu kwa sababu mambo hayo yamefanyika chini ya utawala wao,” alisema.
Mara baada ya Pinda kuzungumza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, alisema hatua ya kujiuzulu na ripoti hiyo inafungua milango ya sheria kuchukua mkondo wake kwa wale wote waliohusika.
“Pia tunaomba Bunge liridhie uundaji wa tume ya uchunguzi wa kimahakama ambayo tuna hakika itayaangalia mambo yote yaliyotokea kwa kina zaidi,” alisema.
Kabla ya kujiuzulu
Baadhi ya wabunge walilazimika kukatisha uchangiaji wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyochunguza tuhuma za mauaji katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Wabunge walichangia hoja hiyo katika hali ya huzuni, huku wengi wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mawaziri wengine wanne wajiuzulu.
Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mathayo David Mathayo, Waziri wa Ulinzi Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Hali hiyo ilitokea baada ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, kuwasilisha taarifa iliyobainisha unyama wa kutisha waliotendewa wananchi wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.
Akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, Lembeli alisema wamebaini askari waliohusika katika operesheni hiyo walikiuka misingi ya ubinadamu, ikiwemo kutesa, kuharibu mali, kuwaua watu pamoja na mifugo.
“Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilitakiwa kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti katika Mkutano wa Kumi na Nne
(14) wa Bunge. Hivyo basi, baada ya uteuzi huo, wajumbe wa Kamati Ndogo  walipanga kuanza kazi Novemba, 25 mwaka huu na kuikamilisha ifikapo Desemba 15, 2013,” alisema.
Lembeli, alieleza kuwa Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilitekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na hadidu za rejea za  kusoma na kuchambua nyaraka zilizoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Alibainisha pia waliangalia mpango kazi wa operesheni hiyo, tathmini ya utekelezaji wake, sheria ya kinga, maadili na madaraka ya Bunge (Na.3) 1988, sheria ya wanyamapori (Na. 5) 2009, kanuni za kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2013.
Alisema katika kuifanya kazi hiyo, pia walipata fursa ya kuwahoji watu mbalimbali ambapo walibaini udhalilishaji mkubwa miongoni mwa jamii.
Alibainisha kuwa kamati ilibaini tatizo la ujangili ni kubwa na lilisababisha idadi ya tembo iendelee kupungua nchini.
“Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya tembo imepungua kutoka 350,000 (miaka ya 1970) hadi kufikia 55,000 (mwaka 1989), juhudi za kukabiliana na hali hiyo kupitia operesheni zilizowahi kutekelezwa huko nyuma zilisaidia kuongeza idadi ya tembo hadi 141,000 (mwaka 2006) ingawa ilishuka tena hadi kufikia 110,000 (mwaka 2009),” alieleza Lembeli.
Alisema katika zoezi hilo askari waliwatesa watuhumiwa na kuwasababishia maumivu, ulemavu, vifo na uharibifu wa mali.
Aliongeza kuwa kamati ilikutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Kagasheki na baada ya mahojiano walibaini baadhi ya watendaji wa juu wa wizara walidaiwa kukwamisha utekelezaji wa maagizo yake.
“Baadhi ya waheshimiwa wabunge kutuhumiwa kujihusisha na vitendo  vya ujangili na biashara haramu ya nyara za serikali. Baadhi ya mawaziri kutoa kauli zenye kuingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, mfano kutoa maelekezo kwa wahusika wa Operesheni Tokomeza kwamba wasiguse viongozi wa kisiasa wa ngazi zote.
“Baadhi ya viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kushiriki kudhoofisha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kusindikiza au kusaidia watuhumiwa wa ujangili kutoroka. Mfano viongozi wa polisi wa wilaya na mikoa,” alieleza.
Alisema baadhi ya waathirika walitoa ushahidi na vielelezo vya maandishi na picha ili kuthibitisha yale waliyokuwa wakiyaeleza mbele ya Kamati
Yaliyobainika
Lembeli alisema ulibainika unyama mkubwa ikiwemo viongozi, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watumishi wa serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza.
“Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao,” alisema.
Alisema Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanae wa kiume akishuhudia.
“Pia alidai kulazimishwa kuchora picha ya chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake. Vilevile, Neema Moses wa Babati alidai kuvuliwa nguo na kulazimishwa afanye mapenzi na wakwe zake na pia kuingizwa chupa sehemu zake za siri.
“Baadhi ya akina mama walidai kubakwa na kulawitiwa. Mfano; katika Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga, mwanamke mmoja alidai kubakwa na askari wawili wa Operesheni Tokomeza Ujangili mida ya usiku.
“Vilevile, mama mmoja mkazi wa Kata ya Matongo wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu wa Operesheni Tokomeza Ujangili huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki,” alisema.
Alibainisha kuwa baadhi ya watuhumiwa waliopelekwa katika kambi za mahojiano walidai kuteswa na kupewa adhabu zinazokiuka haki za binadamu ikiwemo kuvuliwa nguo zote.
“Mfano Diwani wa Kata ya Sakasaka Wilaya ya Meatu, Peter Samwel, alidai kuadhibiwa akiwa mtupu kwa kupewa adhabu za kijeshi kama kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti,” alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na ukatili mkubwa, baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina ya Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti).
Aliongeza kuwa pia operesheni hiyo iliongozwa kwa rushwa ambako wananchi walidai kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa watumishi wanaosimamia mapori ya akiba ya Maswa, Kigosi, Moyowosi, Burigi, Kimisi na Mkungunero.
Wachangiaji
Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah (CCM), ambaye alikuwa wa kwanza kuchangia taarifa hiyo iliyoonyesha operesheni hiyo ilivyoendeshwa kwa ukatili wa hali ya juu kiasi cha kuwafanya baadhi ya wabunge kutoa machozi.
Shah, alibainisha hakuna sababu ya Waziri Mkuu Pinda na mawaziri wa wizara husika kutojiuzulu mara moja kutokana na ukatili wa hali ya juu waliotendewa Watanzania, ikiwemo kuuawa kinyama, wanawake kubakwa na wengine wakilazimishwa kufanya mapenzi na mama au watoto wao.
Huku akionyesha picha za namna watu walivyouawa kikatili, Shah alisema askari waliua watu ovyo na watoto walilazimishwa kuzini na wazazi wao mbele ya wakwe, wakidaiwa kuwa majangili na kuhoji ni operesheni ya aina gani hiyo.
Alisema pamoja na operesheni hiyo ya kikatili mno, hakuna mfugaji hata mmoja aliyekutwa na meno ya tembo, na kuongeza kwamba yote hayo yametokea kutokana na kuwepo watendaji wabovu katika serikali.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alihoji sababu za mawaziri wa wizara zilizohusika na operesheni hiyo kubaki madarakani huku nchi ikiwa katika fedheha kubwa.
“Inasikitisha sana kuona mtu anaambiwa atembee na swala aliyekufa na wengine kufikia mbali kuwataka wawaingilie wanyama, tunaipeleka wapi nchi hii jamani?” alihoji mbunge huyo.
Nkumba alitaka watendaji wa vyombo vya dola waliohusika katika ukatili huo wafukuzwe kazi na kufunguliwa mashitaka kutokana na makosa makubwa ya kuwadhalilisha wananchi.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alilitaka Bunge lichukue uamuzi wa kumwondoa Waziri Mkuu bila kusita ikiwa atagoma kujiuzulu kwa hiyari yake.
“Sisi kama Bunge hatuna nguvu ya kuwatoa mawaziri, bali tuna uhuru wa kumtoa Waziri Mkuu na ikumbukwe kwamba hata Mwinyi wakati ule hakufanya makosa na ndivyo namtaka Waziri Mkuu afanye, kama hawezi Bunge lichukue hatua,” alisisitiza Zitto.
Zitto, alisema ni aibu kubwa kwa askari waliotakiwa kulinda raia wanatesa na kubaka wanawake, hivyo akalitaka Bunge lichukue hatua za kuwatetea waathirika.
“Watanzania hao hao ndio wamekuwa wakikatwa kodi zao kwa ajili ya kuwavisha, kuwalisha na kuwapatia silaha  askari wetu, lakini leo hii ndio wanaoongoza kuwanyanyasa na kuwaua,” alisema Zitto.
Zitto adai kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ilikiri kulikuwa na ukatili dhidi ya mifugo na wananchi kiasi cha kusababisha ulemavu au vifo, hivyo hakuna sababu mawaziri kutowajibika.
“Tulitegemea ni operesheni kwa ajili ya kusaidia wananchi, lakini badala yake ikawashughulikia wananchi na mifugo yao.
“Eti mawaziri wajipime, kivipi? Hili jambo ni zito sana, watu wamekufa na hakuna namna yoyote ya kufanya kuonyesha tumekasirishwa na kuuawa na kuteswa kwao, isipokuwa ni serikali kuu kuwajibika, kwa maana ya Waziri Mkuu kuchukua hatua, ili serikali nyingine zinazokuja zijue kuwa akiteswa, akiuawa hata kama ni mtu mmoja lazima wawajibike,” alisema.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), mbali na kuunga mkono hatua ya kutaka waziri mkuu na mawaziri waliotajwa kujiuzulu, alihoji sababu za msingi zilizowafanya wajumbe wa tume kutomhoji Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuzingatia kuwa askari wake waliongoza operesheni hiyo.
Alisema kuwa hata Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, George Mkuchika, anayesimamia usalama wa taifa, naye anastahili kujiuzulu kwa sababu watumishi wake nao walihusika na ukatili huo.
Alihoji pia sababu za Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria na Katiba kutojiuzulu kwa sababu watumishi wa Idara ya Mahakama walihusika katika kusaidia ukatili huo, huku akitaka mahakimu waliohusika kufunguliwa mashitaka.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) alisema Operesheni Tokomeza imeifedhehesha Tanzania anga za kimataifa na kuonyesha kwamba ndivyo nchi hii watu wake walivyo.
Mbatia, alisema tatizo la unyanyasaji wa wafugajii halikuanza jana wala juzi, bali limelelewa kwa zaidi ya miaka zaidi ya ishirini maana hata Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake alishawahi kulalamikia suala la Loliondo.
“Wakati tunapowapa pole Watanzania hawa waliopoteza maisha, tuhakikishe fidia inatolewa na kujiuliza kwanini mauaji haya yanatokea? Mkoani Morogoro kuna mapigano ya wakulima na wafugaji kila siku. Je, tumeshindwa kugawa ardhi vema, hadi watu wanauawa kiasi hiki?
“Mfano, Desemba mwaka jana ukatili wa kinyama ulifanyika chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, nani aliwajibika? Minjingu, kuna kijana mmoja alitolewa Mbauda na kuteswa kwelikweli…Hii inaonyesha wazi kwamba ni mtandao uliosukwa na walionacho na ndiyo maana hata wakubwa hawakuguswa,” alibainisha Mbatia.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema aliamua kuvaa nguo nyeusi kuomboleza vifo vya kikatili vya Watanzania, kwa sababu Operesheni Tokomeza Ujangili iligeuzwa na kuwa Operesheni Tokomeza Ufugaji, na hawataeleweka kwa jamii kama wataamua kufunika kombe mwanaharamu apite, na adhabu yao itakuwa kali kesho mbinguni.
“Taarifa ya Lembeli imeonyesha watu na mifugo ilitokomezwa. Najiuliza wale akina mama waliobakwa na wanaume walikuwa katika hali gani ukizingatia siku hizi kuna ukimwi?
“Kama vile haitoshi, mwanamume alilazimshwa kufanya mapenzi na mti, lini haya yameanza kufanyika jamani? Halafu tumekaa hapa tunataka kufunika kombe, tutahukumiwa ndugu zangu kesho kwa Mola,” alisema.
Alihoji sababu za kupeleka majeshi, bunduki na mabomu kwa raia, na kutendewa ukatili mkuu, akihoji Waziri Mkuu alikuwa wapi wakati watu wanapigwa na kufa pamoja na kupewa kila aina ya vitendea kazi ikiwemo ndege na magari.
“Halafu mawaziri mnataka kupona, mponee wapi? Katika hili Waziri wa Ulinzi ukipona katika Bunge hili, nakuhakikishia mbele ya Mungu hutapona,” alisema.
Lugola alishangazwa na kauli za Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kulalamika kwamba alipokonywa kazi, na kuhoji sababu za kuendelea na kazi.
“Kama rais atashindwa kumfukuza kazi mara moja Waziri Mkuu, basi nitakuwa wa kwanza kuleta hoja bungeni ya kumfukuza Waziri Mkuu,” alisema Lugola.
Waziri kivuli wa nishati na madini, Peter Msigwa (CHADEMA), pamoja na kuungana na wabunge wenzake, alisema wapinzani walidharauliwa mno kila walipokuwa wakihitahadharisha serikali kuhusiana na uzembe.
Alisema wabunge wa upinzani wamekuwa wakionekana wasaliti wanapoishambulia serikali, na kuonekana sio wazalendo.
“Unaweza kuichukia serikali ukaipenda nchi, na kuichukia serikali si kwamba wewe sio mzalendo kwani waweza kuipenda na usiwe mzalendo vilevile.
“Kwa miaka mitatu tumetoa ushauri, lakini tumebezana na kwa kweli Waziri Mkuu mmekuwa na mazoea ya kupuuza mambo ya msingi bila kujali kuwa nchi hii ni yetu wote.
“Tumeshambuliwa na kupeana majina ya ajabu hapa bungeni. Katika hili namtaka Waziri Mkuu kuelewa kwamba hatuna chuki nawe, lakini tunakutaka ujiuzulu.
“Waziri Kagasheki katika operesheni umetoa matamshi mengi yakiwemo kuwaagiza askari wamalizane huko huko…, mara umesema mtandao huu ni mpana na unashindwa, kwanini hujajiuzulu, maana sasa unafanya nini? Ilitegemewa utuambie umechukua hatua gani.
“Leo tunazungumzia damu za watu, na kama tuko makini, waziri mkuu ungekuwa unaandika barua ya kujiuzulu na mawaziri wengine wafuatie. Hizi damu zinawalilia, hatutaki tukichukua nchi tuwapeleke The Hague, jiuzuluni tuwaage kwa heshima,” alisema.
Mbunge wa Longido, Lekule Lazier (CCM), alionya kuwa jambo hilo lisifanywe kisiasa kwa kuwa waliokufa ni Watanzania na amani imetoweka na kuhoji kati ya wafugaji waliouawa nani alikamatwa na meno ya tembo.
Alisema ikiwa waziri mkuu na mawaziri wengine watakataa na Bunge kushindwa kuwawajibisha, basi Bunge livunjwe maana hakuna maana ya kuwa wabunge wa watu wanaopigwa risasi na kuuawa.
Laizer, alisema kama wabunge wasingeagiza tume iundwe serikali ingenyamaza na kuwaonya wale wanaopenda kuleta siasa kuacha kabisa.
Hii ni kamati teule ya tatu kuundwa tangu Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005, ambapo matokeo ya kamati za awali hazikuwaacha viongozi waliotakiwa kuwajibika kuendelea na nyadhifa zao.
Februari 7, 2008 aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujiuzulu baada ya kutajwa katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mkataba tata wa Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Richmond.
Kamati hiyo iliyongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Uchukuzi, ilitumia siku 45 na kuwahoji mashahidi 75, vielelezo zaidi ya mia moja na maswali zaidi ya 2,700.
Mwaka 2012 Bunge liliunda kamati nyingine teule iliyokuwa na jukumu la kuchunguza utaratibu uliotumiwa na Wizara ya Nishati na Madini, kukusanya fedha kutoka katika taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kupitisha bajeti, wakati huo Wizara ya Nishati ilikuwa chini ya William Ngeleja.
Matokeo ya kamati hiyo iliyokuwa chini ya Injinia Ramo Matala Makani ilisababisha Rais Kikwete amuondoe David Jairo katika nafasi yake ya ukatibu mkuu wizara ya nishati na madini.
Hata hivyo, kuondoka kwa Jairo haikuwa nafuu kwa baadhi ya mawaziri kwani Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto alianzisha mchakato wa kukusanya kura za kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Pinda kabla ya kuondoa hoja yake bungeni baada ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya mawaziri kwa baadhi ya wizara.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...