MAASKOFU WATAKA TIMUATIMUA KANISANI

TIMUATIMUA inayoendelea kufanywa na Papa Francis katika benki ya Vatican, imevutia maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini ambao wameshauri katika miradi ya Kanisa hilo nchini, hata kama hiyo ichukuliwe kukitokea kutowajibika.
Wakizungumza na gazeti hili hivi karibuni, maaskofu wa Kanisa hilo nchini walisema hatua aliyochukua Papa Francis ya kuondoa madarakani makadinali wanne waliokuwa wasimamizi wa benki ya Vatican ni nzuri.
Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao alisema mwishoni mwa wiki iliyopita, kwamba hatua hiyo inaendana na sera za Papa alizoingia nazo katika uongozi na hata Kanisa la Tanzania, kukitokea kutowajibika, basi hatua kama hizo zichukuliwe.
“Tumepokea mabadiliko hayo kwa sababu ya sera zake, mtu kama Papa Francis kwa namna alivyoingia, anahitaji watu wa kufikisha sera hizo anapotaka, tunaona ni sawa alichofanya ila kuna mambo hawezi kubadilisha kabisa; tunu ya imani na mafundisho ya imani,” alisema Askofu Shao na kuongeza:
“Hao makadinali ni binadamu kama wengine, siku zote katika madaraka ya chini akiharibu wa juu unawajibika, mfano mawaziri wetu wanne walijiuzulu hivi karibuni, si kwamba walikwenda wenyewe msituni.
“Hapa kwetu katika Kanisa huwa tunawajibishana, lakini tukiona kutowajibika, tufanye uamuzi, mabadiliko ni vizuri yakawepo kila mahali,” alisema Askofu Shao.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Method Kilaini alisema Papa ameonesha mfano wa uwajibikaji na kwamba katika Kanisa hakuna kubebana.

Alisema ingawa wakati kashfa yenyewe ikitendeka katika benki hiyo, inawezekana makadinali hao hawakuwepo katika nafasi hizo, lakini kiongozi yeyote lazima awajibike na kukubali hilo kwa kuwa ndiye mwenye dhamana kwa wakati huo.
“Inawezekana wakati ule wa kashfa hii hawakuwapo, lakini ndio uwajibikaji wenyewe huo, ni kama mawaziri waliojiuzulu, hawakuhusika moja kwa moja na ubakaji wanawake lakini wamliwajibika kama viongozi,” alisema Askofu Kilaini.
Washauri wakali Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, kikosi cha makadinali wa kumshauri Papa alichokiunda baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki duniani Machi 13 mwaka jana, kina watu wakali, ambao hawako tayari kuona jambo lolote linaharibika au Kanisa kuchafuliwa.
Alisema makadinali hao, akiwamo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kadinali Laurent Monsengwo Pasinya, ni viongozi walio tayari kusafisha chochote kisichokuwa sawa ndani ya Kanisa, lakini hatua hiyo haimaanishi wahusika ni wezi bali uwajibikaji. Gazeti hili wiki iliyopita liliandika hatua ya Papa Francis kuwaondoa madarakani makadinali wanne, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya utakatishaji fedha katika benki ya Vatican.
Makadinali waliofutwa kazi ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican, Tarcisio Bertone, Odilo Scherer wa Brazil, Telesphore Toppo wa India na Domenico Calcagno wa Vatican.
Makadinali hao wote waliteuliwa na Papa Benedict XVI muda mfupi kabla ya kujiuzulu na walikuwa na miezi 11 tu ya utumishi wao katika kipindi cha miaka mitano.

Aliyepona katika hatua hiyo, ni Kadinali Jean-Louis Tauran, Mkuu wa Baraza la Upapa linalohusika na mijadala ya kidini. Benki ya Vatican, ilikumbwa na kashfa ya kutakatisha fedha mwaka 2010 baada ya waendesha mashitaka wa Italia kugundua shughuli zenye utata zihusuzo fedha chafu ndani yake.
Tayari watu wa kushika nafasi zao walishateuliwa na Papa.

Hayo ni mabadiliko makubwa kufanywa na Papa Francis, Muargentina na Papa wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,000.
Aidha, mabadiliko makubwa pia yanatarajiwa kufanyika kutokana na kashfa ya udhalilishaji wa kingono unaohusu baadhi makasisi wa Kanisa hilo na hatua tayari zinaanza kuonekana katika usimamizi wa sheria za Kanisa.
CHANZO NI HABARI LEO


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...