LICHA
ya kutangaza kujiuzulu kwa agizo la serikali baada ya ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Uttouh,
kumtia hatiani aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani,
ameng’ang’ania kiti hicho.
Januari 17, mwaka huu, Amani alikubali agizo la Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, baada ya CAG kuthibitisha kuwa miradi aliyokuwa akiitekeleza
katika manispaa hiyo ilikiuka utaratibu na haikuwashirikisha madiwani.
Mbali na Amani, wengine waliowajibishwa kwa kuvuliwa madaraka ni
pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Hamis Kaputa, aliyekuwa
amehamia Mbeya, Mhandisi wa Halmashauri, Steven Nzihirwa na Mhasibu,
Hamdun Ulomy.
Katika hali ya kushangaza, juzi Amani aliandika barua kwenda kwa
mkurugenzi wa manispaa hiyo, akimwarifu kuwa hatakuwepo kwa wiki sita,
hivyo majukumu yake yatatekelezwa na naibu meya.
Nakala ya barua hiyo ya Januari 12, 2014 yenye kumb. Na.
BMC/R.30/MEYA/Vol.II/526, ilitumwa pia kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba,
Katibu Tawala wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa, Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera na
Naibu Meya, Alexander Ngalinda.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka mjini Bukoba jana zilisema
kuwa barua hiyo yenye kichwa cha habari: ‘Yah: Kusafiri kumpeleka mtoto
wangu kwenda kutibiwa,’ ilizua taharuki kwa baadhi ya wakazi wa Bukoba,
wakihoji kama Amani amerukwa akili au la.
Barua hiyo ilisomeka: “Nakujulisha kuwa sitakuwepo kwa takriban muda
wa wiki sita. Nampeleka mtoto wangu kwenye matibabu ya moyo (Congenital
Cardiac Mulfunction).
“Kwa muda ambao sitakuwepo, Naibu Meya afanye majukumu yote ya Meya.
Ikiwa ni pamoja na kuendesha vikao hadi nitakaporudi,” alisaini Dk.
Anatory Amani akijitambulisha kama Meya wa Manispaa ya Bukoba.
Gazeti hili lilimtafuta Amani ili kupata ufafanuzi juu ya barua hiyo
lakini simu yake iliita bila kupokewa, hata ujumbe mfupi alioandikiwa
hakuujibu.
Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe, alisema serikali na jamii kwa ujumla
inatambua kuwa Amani alijiuzulu kama meya Januari 17, baada ya
taarifa ya CAG.
“Kwamba barua aliyomwandikia mkurugenzi imefanyiwa kazi na ngazi
ya serikali ya mkoa na wilaya. Malumbano ya kisiasa yamewachosha
wananchi na kurudisha maendeleo nyuma, kwa sasa basi,” alisema
Massawe.
Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya, Zipora Pangani, alisema hata yeye nakala
ya barua hiyo aliipata jana, hivyo alikuwa bado anafuatilia na kuomba
kwa sasa aulizwe Mkurugenzi, Shimwela L.E, ambaye hakupokea simu wala
kujibu ujumbe mfupi.
Oktoba 30, 2013 CAG na timu yake walianza ukaguzi wa miradi hiyo
katika maeneo mbalimbali, kazi ambayo waliikamilisha na hatimaye kutoa
ripoti yao wiki iliyopita.
Katika ripoti yake CAG alisema uwekezaji wenye mashaka kwenye kituo
cha kuosha magari, zabuni haikuwa shindanishi na kwamba ilikuwa kinyume
cha taratibu.
Alisema kuwa waliosaini mkataba huo ni Khamis Kaputa, aliyekuwa
mkurugenzi na Meya Amani, huku wakijua yalikuwa makosa kufanya hivyo
bila idhini ya kikao cha madiwani.
Uttouh alifafanua kuwa Kamupuni husika ya ASEC iliyofanya kazi hiyo
haijasajiliwa na Msajili wa makampuni (Brela) na hailipi kodi TRA.
Kuhusu tuhuma za upimaji na ugawaji wa viwanja, ripoti ilibaini kuwa
kati ya wananchi 800 waliotakiwa kugawiwa viwanja ni wananchi 300 ndio
waliogawiwa kutokana na migogoro ya viwanja kimila.
“Manispaa iliingia makubaliano na Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT)
kupima viwanja 5,000 kwa kugawana faida ya asilimia 50 kwa 50 na UTT.
“Mkataba huo ulisainiwa na Kaimu Meya, Ngalinda, kwa upande wa
manispaa bila kupata idhini ya Baraza la Madiwani na mkopo huo
ulichukuliwa bila kupata ridhaa ya waziri mwenye thamana,” alisema.
Alisema kuwa mradi huo gharama za faida zilikuwa zinabadilika kila
mara na walikusudia kupata sh bilioni 1.2, lakini ziliongezeka hadi
kufikia sh bilioni 4.8, lakini zilizoonekana kwa CAG ni sh bilioni 4.6,
kwa hiyo sh milioni 200 hazijulikani zilipo.
Uttouh aliongeza kuwa kuhusu tuhuma za matengenezo ya barabara mpya,
Manispaa ya Bukoba iliingia mkataba na mkandarasi aitwaye Kajuna
Investment wa sh milioni 138.
Alisema kuwa mkandarasi huyo alilipwa fedha za dharura ambazo
hazikuwa na nyaraka, hivyo malipo hayo yaliongezwa hadi kufikia sh
milioni 227 kwa kutumia barua iliyosainiwa tofauti na ile ya awali.
“Malipo hayo hayakuwa na idhini ya mkandarasi wa serikali na yalikuwa kinyume cha kanuni za manunuzi ya umma,” alisema.
Uttouh katika tuhuma za mradi wa ujenzi wa soko kuu la mjini Bukoba,
alisema kuwa walibaini kuwa utaratibu haukupata idhini ya madiwani ya
kumlipa mkandarasi mshauri OGM Consultant sh milioni 789.
Alisema sh milioni 200 zilizotumika kumpata OGM Consultant ya Dar es
Salaam hazikufuata utaratibu na mkataba mwingine uliosainiwa kinyume cha
sheria na OGM ni sh milioni 700, ambapo madiwani waliambiwa ni sh
milioni 400 na kampuni hiyo hailipi kodi TRA.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha mabasi Bukoba, CAG alisema mradi huo
haukutangazwa kwenye gazeti la serikali lakini walipata mkandarasi na
kumlipa fedha za kazi hiyo kinyume cha taratibu za serikali.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa bwawa, alisema kuwa haukuwahi kujadiliwa na
baraza la madiwani, kwamba ulikuwa ni mradi wa wajanja. tu.
Suala la posho kwa madiwani katika safari ya mafunzo nje ya wilaya
nalo liliguswa, ambapo madiwani wawili waliolipwa sh 400,000 kila mmoja
hawakusafiri lakini fedha hizo hazikurudishwa manispaa.