WAKILI WA ZITTO ATOA YA MAYONI "HATUSHINDANI NA CHAMA AU WANACHAMA WA CHADEMA"

Wakili msomi AlbertMsando ametoa yaliyo moyoni. Kupitia ukarasa wake wa Fb haya ndio aliyoandika.

By; Albert Msando

Kwa marafiki zangu,

Hatujashinda kesi dhidi ya chama. Hatushindani na chama au wanachama wa CHADEMA.

Natambua kwamba kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA mojawapo ya madhumuni ya chama ni kuendeleza na kudumisha Demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kujenga utamaduni wa demokrasia katika jamii kwa kutambua haki za wengi katika maamuzi na pia kutambua haki za wachache kusikilizwa, kuheshimiwa na kulindwa, sambamba na kukubali ushindani huru, wa haki na wa wazi ....

Pia natambua kwamba kwa mujibu wa Katiba ya chama Wajibu wa mwanachama wa Chadema ni kuwa tayari kupambana na namna yeyote ya uonevu, ukandamizaji, udhalilishaji na ubaguzi.

Wajibu huu ni ndani na nje ya chama. Hatuwezi kutekeleza wajibu upande mmoja. Binafsi ninalo jukumu kutekeleza wajibu wangu kwa manufaa ya chama.

Kumekuwa na lawama, shutuma na malalamiko kwamba nilichokifanya kinadhoofisha chama. Napinga kwa nguvu zangu zote. Inawezekana kabisa nilichofanya kinadhoofisha watu wachache ndani ya chama ila sio CHAMA.

CHADEMA sio mtu binafsi. Ni taasisi. Wanachama wake ndio nguzo muhimu. Sio Zitto wala Mbowe wala Slaa. Hawa ni viongozi tu ambao wajibu wao ni kuendelea kujenga chama.

Uwezo wao upimwe kwa matokeo ya sasa. Sio kwa mvuto na haiba zao. Fundisho la haya yote ni moja: KUVUMILIANA SIO KUFICHIANA SIRI AU UDHAIFU. Kosa limetendeka na kukubali kosa sio dhambi.

Ni wazi kabisa kumekuwa na kutokuelewana kwa muda mrefu. Ni dhahiri viongozi wetu wamekuwa wanajua udhaifu wa kila mmoja wao. Lakini kwa sababu ambazo hazijawa wazi waliamua kukaa kimya. Au labda ilikuwa ni kwa kuamini kwamba yatamalizika bila athari. Sasa matokeo yake ndio haya.

Kinachohitajika sasa sio kutafuta mchawi. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha suluhu inapatikana. Na niseme wazi kabisa, kama suluhu ni mtu kufukuzwa basi tuhakikishe hilo linafanyika kwa mujibu wa Katiba na Kanuni kwa kuzingatia haki za msingi kama ambavyo tumekuwa tukipigania.

Haki itendeke, na zaidi lazima ionekane imetendeka. Pamoja tunaweza.

Mwisho, tusiruhusu muendelezo wa 'ufuasi' wa watu ndani ya chama. Tuwe wafuasi wa misingi ya chama. Bado nafasi ipo ya kurekebisha pale tulipoangukia kama busara na hekima vitatumika.

Nawatakia kila kheri ndugu zangu.

"In a battle for the minority rights we have to promote the rights of the majority and we will remain united" AGM 2014.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...