Waziri
mkuu wa Finland Jyirk Katainen ameingia katika siku ya pili ya ziara
yake ya kikazi nchini Tanzania kwa kutembelea bandari ya Dar es Salaam
na kuongeza kuwa nchi yake pamoja na umoja wa ulaya inaunga mkono mpango
wa serikali wa matokeo makubwa sasa na kwamba bandari za kisasa
zinazotoa huduma kwa wakati ni muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi
yeyote duniani.
Ni siku ya pili ya kuwepo kwake hapa nchini
Tanzania waziri mkuu wa Finland Jyirk Katainen ambapo katika siku hii
anatembelea bandari ya Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya bandari
hiyo na baadae kupata fursa ya kuzungumza na baadhi ya viongozi wa
serikali na watendaji wa bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza na viongozi hao mara baada ya
kutembezwa bandarini hapo waziri mkuu huyo pamoja na mambo mengine
amesema kuwa nchi yake pamoja na bara la ulaya inaunga mkono Tanzania
katika mpango wake wa matokeo makubwa sasa katika sekta ya miundo mbinu
ikiwa ni pamoja na kuiboresha bandari ya Dar es Salaam na kuongeza kuwa
bandari za kisasa zinazotoa huduma kwa wakati ni kichocheo kikubwa cha
ukuaji wa uchumi.
Akizungumza katika mkutano huo balozi wa umoja wa
ulaya hapa nchini Mh Filiberto Sebregondi amesema kupitia mpango wa
serikali wa matokeo makubwa sasa tayari mabadilko yameanza
kujidhihirisha katika bandari ya Dar es Salaam na kwamba jitihada zaidi
zinahitajika ili kuiwezesha bandari hiyo kupokea na kusafirisha bidhaa
nyingi zaidi.
Kwaupande wake waziri wa uchukuzi wa Tanzania Mh
Harrison Mwakyembe ameitumia fursa hiyo kumueleza waziri mkuu huyo
matokeo ya mkutano wa jukwaa la kimataifa la uchumi uliofanyika hivi
karibuni Davos nchini Uswis kuwa katika miradi 51 iliyowasilishwa katika
mkutano huo kwa ajili ya kupewa kipaumbele na kuendelezwa kama mfano wa
ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya miundo mbinu barani Afrika
mradi wa ukanda wa uchukuzi wa kati ulioko Tanzania umeteuliwa.