Arusha, Tanzania.
Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
mkoani Manyara, Paulina Gekul LEO, ameshambuliwa na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Babati, Omari Mkombole na mbunge huyo kulazimika
kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao wameingilia kati sakata hilo.
Katika vurugu zilizotokana na Mbunge
wa Chadema kupigania maslahi ya Wananchi, pia Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo Mohamedi Fara naye ameshambulia wakati wakigombea kabrasha lenye
majina ya wananchi wanaopaswa kupewa ardhi.
Katika pukurushani hizo Gekul amesema
amechaniwa nguo zake, na kwamba amedhalilishwa na kuporwa fedha zaidi ya
Sh5 milioni zilizokuwa kwenye mkoba wake.
Vurugu hizo ziliibuka baada ya
kumalizika kwa kikao kilichofanyika chini ya mkurugenzi huyo kwenye
Ukumbi wa Halmashauri ya Babati.
Baada ya mbunge huyo kushambuliwa
alikwenda polisi kutoa taarifa za kushambuliwa na vigogo hao wa
halmashauri na kuweka wazi kuwa kiini cha vurugu hizo zilitokana na
kikao cha kujadili ugawaji wa shamba la Sisal Plantation lenye ekari
4200.
Vyanzo vya habari vimebainisha kuwa
awali vigogo hao wa halmashauri hiyo walimpokonya nyaraka ambazo
walidhania zilikuwa na majina ya wananchi ambao wanatarajiwa kugawiwa
viwanja, lakini walipobaini karatasi au nyaraka walizpora hazina majina
ya wananchi hao walimfuta huku akijaribu kutoka nje na kumfungia ndani
ya ukumbi wa Babati na kumpora pochi yake na kutoa nyaraka pamoja na
kuchukua fedha.
Chanzo kingine kimebainisha kuwa awali
wakati kikao hicho kikiendelea inasemekana mbunge huyo alibaini katika
nyaraka ambazo zimekusudiwa na halmashauri kutumika wakati wa kugawa
shamba hilo zilikuwa zimechomekewa majina ya maofisa mbalimbali na
kuwaacha wananchi wengi bila kuwapo kwenye mpango wa mgao huo.
Taarifa zinaeleza baada ya mbunge huyo
kuonekana kushtukia mchezo huo ndiyo vigogo wa halmashauri walifunga
mlango na kumpora nyaraka hizo.
Imeelezwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Babati wakati akizungumzia sakata hilo amesema mtu yoyote amempiga mbunge huyo.
Kuhusu, Mkurugezi wa Halmashauri hiyo
hajasema lolote mpaka sasa licha ya waandishi wa habari kumtaka atoe
maoni yake kuhusu sakata hilo.