KAMATI kuu ya chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) imemteua aliyekuwa mshindi wa pili wa kura za maoni katika zoezi la kura za maoni Bi Grace Tendega kupeperusha bendela ya Chadema katika uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kamati kuu ya Chadema iliyoketi jijini Dar es Salaam leo zinadai kuwa aliyekuwa mshindi wa kura za maoni mwanasheria Sinkala Mwenda hajateuliwa na kamati kuu hiyo mbali ya kuongoza kwa kura kura 132 dhidi ya kura 122 alizopata mpinzani wake wa karibu Grace Tendega
Katibu wa Chadema wilaya ya Iringa vijijini Felix Nyondo ameuthibitishia mtandao huu wa www.matukiodaima.com kuwa amepata taarifa hizo za kuteuliwa Bi Grace Tendega kuwa mgombea wa Chadema jimbo hilo la Kalenga .
Hata hivyo alisema anapongeza maamuzi ya kamati kuu na kuwataka wana Chadema Kalenga kujiandaa kwa kampeni za uchaguzi huo na kuanza kumnadi mgombea wao ili kuweza kushinda uchaguzi huo mdogo.
Kutokana na uteuzi sasa Tendega atavaana Godfrey Mgimwa wa CCM katika uchaguzi huo ili kuziba nafasi iliyoachwa waziri na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kalenga marehemu Dr Wiliam Mgimwa aliyefariki mwanzoni mwa mwaka huu.
Hata hivyo duru za kisiasa kutoka ndani ya Chadema zinadokeza kuwa sababu ya kuachwa kwa mgombea huyo aliyeshinda kura za maoni mwanasheria Mwenda ni kutokuwa na mtaji wa watu kwa maana ya kutokubalika ndani na nje ya chama hicho hivyo Chadema kuona kumsimamisha Mwenda ni kulipoteza jimbo hilo.
Huku kwa upande wa mteule wao Bi Tendega amekuwa na sifa ya kugombea katika jimbo hilo kupitia chama cha Jahazi Asilia na kufanya vema japo si kwa kushinda hivyo nin imani yao kupitia Chadema anaweza kufanikiwa kushinda.