MTU anayedaiwa kujiita daktari
mkazi wa Kijiji cha Mudio, Kata ya Masama Mashariki wilayani Hai mkoani
Kilimanjaro, (jina linahifadhiwa), anadaiwa kuwafanyia tohara kwa nguvu
wanaume 28 nyumbani kwake akisaidiwa na kikundi cha vijana
kinachomsaidia kuwakamata kwa nguvu wanaume ambao hawajatahiriwa.
Habari ambazo gazeti hili limepata na kuthibitishwa na watu
mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dkt. Paul Chaote,
daktari huyo bandia amekuwa wakiwafanyia tohara wanaume hao nyumbani
kwake sebuleni.
Mganga Mkuu huyo wa Wilaya ya Hai, Dkt. Chaote alithibitisha
kuwapo kwa daktari huyo bandia, anayedai anafanyakazi katika hospitali
moja kubwa iliyopo mkoani Arusha, jina tunalo.
Alisema madai ya daktari huyo kuwa anafanyakazi katika hospitali
hiyo yalikuwa hayajathibitishwa. Alisema tayari serikali imemzuia mtu
huyo kuwafanyia tohara watu hao kutokana na kuwa daktari bandia.
Habari ambazo zimethibitishwa na mmoja wa maofisa wa polisi
ambaye hakutaka kutaja jina lake alithibitisha daktari huyo bandia
kushikiliwa polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma hizo.
Dkt. Chaote alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba daktari
huyo bandia amekuwa akiwatibu wagonjwa wake hao kwa kutumia duka lake la
dawa, lililopo kijijini hapa licha ya kwamba halitambuliki na mhudumu
wake hana sifa.
“Tulipata taarifa kuhusu kufanyiwa tohara kwa wanaume wa kijiji
cha Modio na baada ya kufuatilia tulibaini ni kweli na tulipomhoji,
(daktari bandia) alidai ni daktari msaidizi katika hospitali iliyopo
mkoani Arusha.
Alisema baada ya taarifa za tukio hilo walifuatilia kijijini
hapo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kubaini nyumba na vifaa
vilivyokuwa vikitumika kufanya tohara. Alisema vifaa alivyokuwa akitumia
havikubaliki kiafya.
“Tumeanza uchunguzi ili kupata watu waliofanyiwa tohara ili
kujua wanaendeleaje kiafya, hii ni kutokana na aina ya huduma aliyokuwa
akiwapa kuwa haikubaliki kiafya,” alisema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masama Mashariki, Ally Mwanga,
alikiri kutokea kwa tukio hilo akisema limesababisha usumbufu kwa
wananchi, huku wengine wakishindwa kwenda katika shughuli za uzalishaji
mali kwa hofu ya kukamatwa na vijana na daktari huyo bandia ili
wakafanyiwe tohara.
Mwanga alisema alipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi
ya kufanyiwa vitendo hivyo na kutoa taarifa polisi wilayani Hai, ambapo
baadaye uchunguzi ulifanyika na mhusika pamoja na timu yake kukamatwa.
SOURCE:::MAJIRA