Na Joseph Zablon na George Njogopa, Mwananchi
Dar es Salaam. Kiongozi wa
Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amenusurika
kifo na mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Mikidadi, ambaye
yupo mahututi katika Hospitali ya Temeke, baada ya kushambuliwa na watu
wanaodaiwa kuwa na mzozo wa ardhi eneo la Kurasini, jijini Dar es
Salaam.
Mchungaji Mtikila alikumbwa na mkasa huo Ijumaa
wiki iliyopita baada ya kufika katika eneo hilo kwa nia ya kutaka
kuwaondoa watu hao wa familia tatu tofauti ambao wanaishi katika eneo
hilo.
Kipigo hicho ambacho kimemsababishia majeraha ya
kisogoni na hata kushonwa nyuzi tatu kichwani, kuvimba usoni na maumivu
makali mwilini yalitokana na kipigo kutoka kwa familia mbili tofauti
zinazoishi katika eneo hilo ambao wanapinga kuhama.
Pia katika sakata hilo, Mtikila anadai kupoteza
simu mbili, pesa taslimu Sh400,000 na Dola za Marekani 2,000 na siku ya
tukio na alifika hapo akiwa ameongozana na watendaji wa Dawati la Msaada
wa Kisheria katika taasisi yake ya Liberty Fund International.
Kamanda wa Polisi Temeke, Engbert Kiondo alikiri
kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wanalifanyia uchunguzi na taarifa
kamili itatolewa kesho Jumanne.
“Ni kweli suala hilo limeripotiwa hapa na
tunalifanyia uchunguzi na kesho Jumanne nitatoa taarifa rasmi kwa
waandishi wa habari,” alisema Kiondo.
Mtikila alisema, mara baada ya kufika eneo hilo,
alikwenda katika nyumba ya kwanza na kuwakuta walinzi ambao walikubali
na kuondoka katika eneo hilo kwani tayari notisi walikuwa nayo na
walikuwa wanatambua kuwa wanatakiwa kuondoka.Alisema baadaye walikwenda
katika nyumba ya pili ambayo anaishi mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la
Rubein Sanga ambaye hata hivyo vitu vyake vingi akuwa amekwisha
vihamisha.
Alisema wakiwa mbele ya nyumba hiyo gari la polisi
lilifika na wakiwa hawana hili wala lile vijana ambao anawataja kuwa ni
wa Sanga walianza kuwashambulia kwa kutumia nondo na kila aina ya
silaha za jadi.
“Walinipiga sana hadi nikapoteza fahamu na wakawa
wanasema huyo Mtikila bebeni na mumchome moto, walitaka kuniua kwani
walinikwida tai hadi ikakatika,” alisema.
Na kuitaja pia familia ya Evelyne Mboya kuwa
ilishiriki kuwashambulia. Alisema wakati vurugu zinaendelea, ndipo
akatokea mmoja wa jirani wanaoishi katika eneo hilo aliyemtaja kwa jina
la Mikidaki: “Yule bwana alipojaribu kunitetea kuwa nisiendelee kupigwa
alipigwa nondo kichwani na akaanguka na alishambuliwa hadi kuzirai na
hajapata fahamu hadi leo,” alisema.
Mchungaji Mtikila alisema alikuwa ameambatana pia
na walinzi wawili (mabaunsa), wafanyakazi wa dawati lake la msaada wa
kisheria lililopo chini ya taasisi yake ya Liberty Fund International na
mmiliki halali wa eneo hilo, Omar Salum Muhsin ambaye pia alijeruhiwa
mkononi kwa nondo.
Mtikila aliwataja wafanyakazi wake waliojeruhiwa
kuwa ni Hemed Wendo na Gray Mhando na akiwa amezirai alibebwa na
kupandishwa katika gari hadi Kituo cha Polisi Chang’ombe ambako yeye na
wenzake walifunguliwa jalada kwa shtaka la kuingia isivyo halali katika
eneo la watu wengine.