Katika hali
isiyokuwa ya kawaida, shule ya Msingi Unenamwa kata ya Luwumbu wilayani Makete mkoa
wa Njombe imeingia kwenye hali ya sintofahamu baada ya mwalimu mkuu wa shule
hiyo kudaiwa kufungua baa shuleni hapo
Tukio Hilo la aina
yake limeonekana kuwachefua wananchi Kwa kuwa si kawaida kutokea kitendo kama hicho kufuatana ma maadili ya taaluma ya ualimu
Akizungumzia suala
hilo mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha
Unenamwa Bw. Labson Tweve amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema biashara hiyo ya baa shuleni
hapo imedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja
“Ndugu mwandishi
wa habari ni kweli kabisa mwalimu huyo amekuwa akiuza pombe kwenye nyumba yake
(nyumba ya mwalimu iliyojengwa na serikali), na anauza bia na pombe za kienyeji
ikiwemo Msabe” amesema Mwenyekiti huyo
Amesema watu
mbalimbali wamekuwa wakijiendea kwenye nyumba ya mwalimu huyo kwa ajili ya
kununua na kunywa pombe kwa kuwa wameshazoea eneo hilo kuwa ndipo wanapojipatia huduma
Naye mwenyekiti wa
kamati ya shule hiyo Bw. Nyaluke Haruni amesema walishawahi kumwita mwalimu
huyo kwenye vikao vya kamati yake na kumuonya pamoja na kumzuia kuuza pombe
kwenye nyumba hiyo ambapo aliacha kuuza hadharani na badala yake akaamua kuuza
kwa siri
“Ukienda kama
mtafiti si rahisi kugundua lakini mteja akienda kwenye nyumba hiyo anapatiwa
huduma anayoitaka (huduma ya pombe) halafu anaondoka” alisema
Wakizungumza kwa
masharti ya kuhifadhiwa majina yao, baadhi ya
wananchi waliozungumza na mwandishi wetu wamesema wananchi wamekuwa wakijiendea
nyumbani kwa mwalimu mkuu huyo kununua pombe na suala hilo limekuwa likiendelea kukua siku hadi
siku
“Ni kweli idadi ya
watu wanaokwenda kwenye nyumba ya mwalimu huyo kununua na kunywa pombe ni kubwa
ingawa wapo wanaokwenda kwa kujificha na wengine wanakwenda bila woga” walisema
wananchi hao wanaoizunguka shule hiyo
Akizungumzia
tuhuma hizo mwalimu mkuu wa shule hiyo Mwl. Evalisto Johanes amekanusha vikali
tuhuma hizo zinazoelekezwa kwake na kusema yeye hajawahi na hafanyi biashara
hiyo ya kuuza pombe nyumbani kwake
Mwl. Johanes
amesema yeye kama mwalimu mkuu anatambua
maadili ya kazi yake kuwa hayaruhusu kuuza pombe shuleni, na yeye anauza vitu
vidogo vidogo kwa wateja wake ambavyo si pombe
“Hilo
jambo si la kweli ndugu mwandishi, mimi siuzi bia wala pombe za kienyeji na
badala yake natoa mahitaji madogo madogo, kama
soda na hizi ni kwa ajili ya wageni wangu wanaonitembelea hapa nyumbani”
alisema mwalimu mkuu huyo
Amesema watu
wasizungumze maneneo ambayo hawana uhakika nayo, na kuongeza kuwa nyumbani
kwake hakuna huduma yeyote ya kilevi inayotolewa na yeye
Afisa elimu shule
za msingi wilaya ya Makete Bw. Antony Mpiluka akitolea ufafanuzi sakata hilo amesema kiutaratibu
hairuhusiwi mwalimu kuuza pombe kwenye eneo la shule na endapo atafanya hivyo
anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kufuata ngazi husika kuanzia chini hadi juu
Bw. Mpiluka
amesema anashangazwa na serikali ya kijiji ambao ndio wamiliki wa shule hiyo
kulifumbia macho suala hilo kwa zaidi ya mwaka
mmoja, na mwenyekiti wa kijiji ambaye ndiye mwenye mamlaka ameshindwa kulitolea
maamuzi suala hilo
na badala yake anakuwa mlalamikaji
“Shule hiyo ipo
chini ya serikali ya kijiji, kama mwalimu huyo anauza pombe shuleni wao ndio
walitakiwa wawe wa kwanza kumuita na kumhoji na baadaye wachukue hatua,
wakishindwa waandike barua wilayani kwa ajili ya hatua zaidi na si wao kama serikali ya kijiji ambayo inamamlaka zote inageuka
kulalamika badala ya kutenda, wao ni watendaji na si walalamikaji” alisema
Mpiluka