MAUAJI YA KIKATILI...KIGOGO MAGEREZA ATEKWA, ATESWA, AUAWA....!!FUATILIA ZAIDI HAPA....

KIGOGO wa cheo cha juu katika Jeshi la Magereza Tanzania, SP Barnabas Nkuba (56) ameuawa kikatili kisha mwili wake kuburuzwa na kutupwa kwenye choo cha nje cha nyumba yake, Uwazi limeichimba.
Jeneza lenye mwili wa marehemu, SP Barnabas Nkuba (56) likiwa limebebwa na maofisa wa Jeshi la Magereza Tanzania.

Tukio hilo lililoacha maswali mengi lakini majibu kiduchu huku jeshi la polisi likihaha kuwanasa wauaji, lilijiri Machi 20, mwaka huu nyumbani kwake, Kitunda -Machimbo, Ilala jijini Dar es Salaam. 

MAZINGIRA YA KUUAWA
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka Jeshi la Magereza, Ukonga, Dar alikokuwa anafanyia kazi mpaka kifo chake, huenda marehemu alitekwa kwanza, kisha akateswa na baadaye kuuawa kikatili.
“Ukiangalia mazingira yanaonesha bosi (marehemu) alitekwa kwanza, akateswa sana na baadaye kuuawa,” kilisema chanzo hicho huku kikiangua kilio cha utu uzima.

MWILI WAKUTWA CHOONI
Habari zaidi zinadai kuwa baada ya kumuua, watu hao waliuburuza mwili hadi kwenye choo cha nje ambako waliutupa ndani yake.

Ndugu na jamaa wa marehemu wakiomboleza msiba wa kigogo huyo.
Wengine walipingana na kauli hiyo, wakisema kuwa huenda afande huyo alipotekwa aliteswa kwanza kisha akaburuzwa hadi chooni akiwa hajiwezi ambako aliuawa.
“Mimi napingana na madai kwamba aliuawa kisha mwili wakautupa chooni kwa sababu, mwili ulikutwa chooni ndiyo lakini pembeni yake kulikuwa na vipande viwili vya matofali ambavyo huenda vilitumika kumpigia marehemu hadi kufa, maana mwili wake ulikutwa na jeraha usoni,” kilisema chanzo kingine.
KUNYONGWA KWATAJWA
Taarifa zingine zilidai kuwa marehemu ni kama alinyongwa kwanza kisha kupigwa na  tofali hali iliyosababisha kifo chake cha kimyakimya bila kupiga kelele kwa vile matofali yaliyokutwa chooni hayakuwa na ukubwa wa kutumika kumpigia mtu hadi kufa.
 
Marehemu, SP Barnabas Nkuba enzi za uhai wake.
SAA CHACHE KABLA YA KIFO
Vyanzo vingine vya habari vilisema kwamba siku ya tukio, marehemu alipotoka kazini alipitia dukani na kununua soda mbili ambazo polisi walizikuta mezani sebuleni zikiwa zimenywewa nusu.

MKEWE AHUSISHWA, AKAMATWA, KWA NINI?
Habari zaidi zilisema kwamba marehemu Nkuba alikuwa akiishi na mkewe, Cheula  tu kwani watoto wao walikuwa masomoni.

Inasemekana kwamba marehemu alikuwa na mazoea ya kutangulia kufika nyumbani kabla ya mke wake kwa vile mwanamke huyo anafanya biashara ya kuuza chakula Ukonga-Mazizini, Dar na hurudi nyumbani usiku mwingi.
Ikadaiwa kuwa siku ya  tukio, mwanamke huyo aliwahi kurudi akiwa amepanda bodaboda.
“Mkewe ambaye ni mdogo, maana alimuoa baada ya mke mkubwa kufariki dunia, alipokaribia kwake na bodaboda inadaiwa alimwambia dereva kuwa asifike nyumbani kabisa kwa vile hali si shwari.
“Tunasikia kwamba aliposhuka alikwenda mwenyewe nyumbani kwake na kukuta mlango uko wazi. Akaingiwa na hofu.

“Basi, akaenda baa ya jirani na kuwaambia anaowajua kwamba amefika nyumbani na kukuta mlango uko wazi na kila akiipiga simu ya mumewe, haipatikani.
“Ndipo majirani hao na mwanamke huyo wakaenda nyumbani hapo na kuingia. hawakukuta mtu, hata walipoita Nkuba, Nkuba, wapi! Kimya!

“Walikwenda uani ambako walikuta alama za mburuziko wa kitu, wakazifuata hadi chooni ambako waliukuta mwili wa kigogo huyo akiwa ameshafariki dunia na ndipo polisi walipopewa taarifa.
“Mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Amana, baadaye wakauhamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” kilisema chanzo.

Polisi walipofika, habari zinadai kuwa walimkamata mwanamke huyo kutokana na mazingira yenye utata.
“Tunasikia polisi walishangaa kama yeye ndiyo mwenye nyumba iweje akute mlango wazi ahofie kuingia wakati wanaishi wawili tu? Kwa nini asiingie na kumuita mumewe, pengine alipitiwa na usingizi?

“Halafu kingine, ni kwa  nini alimwambia dereva wa bodaboda asimfikishe nyumbani hali si shwari? Ni hali gani hiyo ambayo haikuwa shwari wakati alikuwa hajaingia ndani?” kilihoji chanzo hicho.
Kwa cheo cha marehemu, angekuwa JWTZ nafasi yake ni meja, kwa jeshi la polisi angekuwa kamanda wa polisi wa wilaya (OCD).

Mwili wa marehemu Nkuba ulisafirishwa Machi 22, mwaka huu kupelekwa Shinyanga kwa mazishi. Ameacha watoto wanne. Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.
-UWAZI


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...