Baadhi
ya wasafiri na wanakijiji wakitizama daraja la Kirurumo lililoharibiwa
kwa mafuriko na kukata mawasiliano kati ya Karatu, Ngorongoro na
Serengeti.
Mamia ya wasafiri waliokuwa
wakitokea Karatu kuelekea Arusha, Dar es Salaam na maeneo mengine ya
nchi, wameshindwa kuendelea na safari baada ya kushindwa kuvuka mto
Kirurumo uliopo mpakani mwa Wilaya za Karatu na Monduli, baada ya mto
huo kufurika na kufunika barabara kutokana na mvua za masika
zinazoendelea kunyesha.
Mwandishi wa habari wa TBC
aliyeko Manyara ameripoti kuwa miongoni mwa watu waliokwama ni pamoja na
watalii waliokuwa wakitoka katika hifadhi za Taifa za Serengeti na
Ngorongoro, na abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi la Dar Express
ambalo lililazimika kurejea mjini Karatu kwa kushindwa kuvuka mto huo.
Abiria wengine waliokuwa
wakisafiri kwa basi la Sai Baba kuelekea jijini Dar es Salaam nao
hawakuweza kuendelea na safari yao kutokana na marufiko hayo.
Mto huo umekuwa ukiporomosha mawe makubwa kutoka milima ya Mbulu Mbulu
Dereva wa Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro, Juma Mushi, ameponea chupu chupu kupoteza uhai katika
mafuriko hayo, baada ya gari aina ya Toyota Land Cruiser SU 36037
kusombwa na mafuriko hayo katika mto Marera, nje kidogo ya mto wa
Karatu, na kukokotwa kwa umbali wa kilometa 70 kutoka barabarani.
Katika jitihada za kujiokoa, dereva huyo alilazimika kutoka kwenye gari lake na kupanda juu ya mti.