KOCHA
wa zamani wa Barcelona, Tito Vilanova amefariki dunia akiwa na umri wa
miaka 45 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani kwa muda mrefu.
Alipelekwa chumba cha dharula jana kwa upasuaji baada ya hali yake kugeuka na kuwa mbaya wiki iliyopita.
Vilanova amekuwa akisumbuliwa na saratani tangu Novemba mwaka 2011 na Radio Nacional imesema alikuwa katika wakati mgumu siku mbili hizi.
Washindi: Vilanova (kushoto) na Eric Abidal (kulia) wakiinua taji la La Liga mwaka 2013
Kocha huyo alilazimika kujiuzulu mwaka 2013 baada ya kuanza kuzidiwa na maradhi hayo.
Timu
yake ilishinda taji la La Liga, lakini Jordi Roura aliifundisha
Barcelona kwa miezi miwili wakati Vilanova aliposafiri kwenda New York
kwa matibabu ya saratani, kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Tata
Martino msimu huu.
Vilanova
aliteuliwa kuwa kocha wa Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2011-12 na
akawawezesha Blaugrana kusawazisha rekodi ya Real Madrid kumaliza msimu
na pointi 100. Alianza kuwa Msaidizi wa Pep Guardiola mwaka 2008.
WASIFU WA TITO VILANOVA...
1968: Kuzaliwa Septemba 17 mjini Bellcaire d'Emporda, kijiji kilichopo Katalunya.
1988: Alijiunga
na timu ya vijana ya Barcelona pamoja na kiungo mwenzake Pep Guardiola,
lakini hakupanda kikosi cha kwanza akichezea kwa miaka miwili Barcelona
B.
1990: Alijiunga na timu ya daraja la chini Figueres.
1992: Alihamia timu ya La Liga, Celta Vigo, lakini akashindwa kupata nafasi kikosi cha kwanza.
1995: Aliondoka Celta.
2002: Alistaafu soka baada ya kucheza madaraja ya chini katimu za Badajoz, Real Mallorca, Lleida, Elche na hatimaye Gramenet.
2007: Baada
ya kufanya kazi kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Tarrassa, Vilanova
akateuliwa kuwa Msaidizi wa Guardiola Barcelona B, ambao kwa pamoja
waliiwezesha timu hiyo kupanda daraja la pili.
2008: Juni
- Guardiola alipewa Ukocha Mkuu wa Barcelona na Vilanova akawa Msaidizi
wake. Wawili hao walishinda taji la Kombe la Mfalme, La Liga na Ligi ya
Mabingwa katika msimu wao wa kwanza kazini. Mataji mawili zaidi ya
ligi, lingine la Ligi ya Mabingwa na mawili ya Klabu Bingwa ya Dunia
yalifuatia.
2011: Novemba
22 - alikwenda kufanyiwa upasuaji wa kwanza wa matatizo yake ya kiafya
akiwa Barcelona na akatumia wiki tatu kabla ya kupona na kurejea kazini.
2012: Aprili 27 - Aliteuliwa kuwa kocha mpya wa Barcelona, baada ya Guardiola kutangaza hataongeza mkataba.
Juni 15 - Vilanova alisani Mkataba wa miaka miwili .
Desemba 19 - Barcelona ilitangaza Vilanova atakwenda kufanyiwa upasuaji kwa mara ya pili na atakosekana kwa wiki sita.
2013: Machi 26 - Baada ya wiki 10 za matibabu New York, Marekani Vilanova alirejea Barcelona.
Aprili 6 - Alirejea Uwanja wa Nou Camp akiiongoza timu hiyo kushinda 5-0 nyumbani dhidi ya Real Mallorca.
Aprili
26 - Alizungumza na vyombo vya habari kwa mara ya kwanza baada ya
matibabu yake, akisema: "Najisikia mwenye furaha na nguvu na ninataka
kuendelea msimu ujao."
Mei 11 - Barcelona ilitwaa taji la 22 la La Liga baada ya wapinzani wao, Real Madrid kukamatwa kwa sare na Espanyol.
Julai 19 - Barcelona ilitangaza kung'atuka kwa Vilanova ili kuendelea na matibabu.
2014: Aprili 25 - Barcelona ilitangaza kifo cha Vilanova akiwa na umri wa miaka 45